Vikundi 33 vyapewa mikopo ya mamilioni

20Jul 2019
Peter Mkwavila
CHAMWINO
Nipashe
Vikundi 33 vyapewa mikopo ya mamilioni

VIKUNDI 33 wilayani Chamwino vimepata mikopo ya Sh. milioni 105.1 zinazotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Kati ya vikundi hivyo, 23 ni vya wanawake, vinane vya vijana na viwili vya walemavu.

Akizungumza katika ziara yake ya kutembelea vikundi hivyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai, alivitaka kuelekeza fedha hizo kwenye malengo yaliyokusudiwa ili mikopo hiyo iwe fursa ya kuwainua kiuchumi wananchi.

Ofisa huyo aliwataka waliopata mikopo hiyo kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuwa na soko la uhakika na wahakikishe wanarejesha mikopo kwa wakati.

“Rejesheni mikopo kwa uaminifu na mkope tena, pia muwatafute mabinti waliozaa wakiwa chini ya miaka 18 ili nao wajiunge kwenye vikundi vya vijana ili kupata mikopo na kujiinua kiuchumi," aliagiza.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Ujirani Mwema kilichonufaika na mikopo hiyo, Sarah Chimangha, alisema kina wanachama 29 na wamepata mkopo wa Sh. milioni 2.5 ambao anaamini utawasaidia kuendesha shughuli zao ikiwamo kufungasha chumvi kwenye vifungashio vyenye ubora.

Stella Madelemu, kiongozi wa Kikundi cha Tubebane kilichoko Kijiji cha Mahama, Kata ya Chilonwa, alisema ni mara yao ya kwanza kupata mkopo na watahakikisha wanaboresha kazi zao.

Alisema wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha alizeti na ufugaji na mkopo wa Sh. milioni 1.5 walioupata utasaidia kuboresha kazi zao za kila siku.