Vikundi vya kuweka, kukopa vyawezeshwa

28May 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Vikundi vya kuweka, kukopa vyawezeshwa

BENKI ya NMB imezindua akaunti maalum kwa ajili ya vikundi vya kuweka na kukopa hususani vya wanawake ili kutekeleza dhana ya kujiwekea akiba na kuwainua wananchi wa kipato cha chini kimaendeleo.

Lengo lingine ni  kuepukana na upotevu wa fedha za vikundi ama kudhulumiana.

Katika taarifa ya benki hiyo kwa umma iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna, alielezwa kaunti hiyo inayojulikana kama ‘NMB Pamoja Account’ imeleta suluhisho kwani ni salama na inaondoa changamoto zote za fedha taslimu kama kudhulumiana na hata kuibiana michango ya wanachama.

“NMB Pamoja Account’ ni akaunti maalum iliyotengenezwa kutoa huduma kwa mahitaji ya vikundi vya kijamii vilevile imetengenezwa kuangalia masuala ya ulinzi na hatari zinazohusiana na kuweka fedha majumbani,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwanakikundi wa Pamoja Akaunti anaweza kutoa michango bila haja ya vikao, kuangalia salio, kuangalia taarifa fupi ya kifedha, kufungua akaunti ya kikundi ya benki kupitia mfumo wa kidijitali au simu janja au simu ya kawaida, kuhamisha fedha  kutoka NMB Pamoja Akaunti ya kikundi kwenda akaunti binafsi za NMB bila makato yoyote.

Alisema akaunti hiyo pia inashirikiana na NMB ChapChap (akaunti ya papo hapo) kufanya miamala kati ya vikundi vyenye akaunti nyingine, na kwamba ushirikiano huo utasaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma za NMB na bidhaa zake kwa karibu zaidi, kwa wateja na wasio wateja wa benki hiyo hasa walio vijijini na  wa vipato vya chini.

Zaipuna alisema kupitia huduma hiyo, wateja wanapata ahueni kwa kutumia simu za mkononi kama njia ya kisasa, huku ikiwapunguzia adha ya kupeleka fedha taslimu ya kikundi benki na pia ya kuhudhuria vikao mbalimbali vya vikundi.

Habari Kubwa