Vikwazo 5 stakabadhi ghalani

16May 2018
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Vikwazo 5 stakabadhi ghalani

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, Augustino Mbulumi, ameiomba serikali kusaidia kutatua changamoto sita zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa stakabadhi za ghala uliofanyika jijini Dodoma jana, Mbulumi alisema changamoto ya kwanza ni bajeti finyu, hivyo kuiomba serikali kuwasaidia kwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya mfumo huo.

“Tuna changamoto ya usafiri, tuna magari mawili tu. Pia tunakabiliwa na changamoto ya kukosa ofisi. Tunayotumia sasa kule Dar es Salaam tunapanga kwa kulipa kodi kubwa,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji huyo aliitaka changamoto ya nne kuwa ni upatikanaji wa soko la uhakika wa mazao, hasa korosho, akiiomba serikali kulipa msukumo suala la kusaka masoko mapya ya mazao yanayozalishwa nchini.

Alisema changamoto nyingine ni hujuma mbalimbali zinazofanywa dhidi ya mfumo huo, akibainisha kuwa serikali haina budi kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa mfumo huo ili wadau wote wawe na lugha moja.

Pamoja na changamoto hizo, Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema mfumo huo umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa asilimia 74 ya uzalishaji wa zao la korosho kulinganishwa na miaka 11 kabla ya kuanzishwa kwa mfumo.

Alisema mfumo huo pia umesaidia nchi kuwa na bei rejea ya korosho na mapato ya kodi kwenye zao la korosho yameongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mbulumi alisema mafanikio mengine ni wakulima kuingia kwenye mfumo rasmi wa kibenki, mifuko ya hifadhi ya jamii na bima za afya.

Aliongeza kuwa mfumo huo pia umewasaidia kuuza mazao yao kwa kutumia vipimo sahihi na uongeza ajira rasmi na zisizo rasmi, akitolea mfano ajira za walinzi wa ghala.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera na Uratibu, Prof. Faustin Kamuzora, aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alisema serikali itazifanyia kazi changamoto zinazoukabili mfumo huo huku akiwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuwashughulikia watu ambao wamekuwa wakiwaibia wakulima kupitia vyama vya ushirika.

“Kama tunataka maendeleo, lazima tuwekeze kwenye kilimo. Kwa kutambua hilo, serikali itaendelea kutunga sheria kali kumlinda mkulima,” Prof. Kamuzora alisema.

Kiongozi huyo wa serikali pia alikiri wafanyabiashara wa mazao ya kilimo wanakabiliwa na changamoto ukosefu wa masoko lakini akasisitiza kuwa tayari Rais John Magufuli ameshaonyesha njia ya kupata masoko nje ya nchi.

Prof. Kamuzora pia alisema anawashangaa watu wanaoupuuza Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ilhali kila anaposhiriki mikutano ya kimataifa ughaibuni, Tanzania imekuwa ikitajwa kuwa nchi ya mfano kwa mafanikio makubwa ya mfumo huo.

Habari Kubwa