Vitambulisho vya machinga vyamtoa ofisini

20Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
MOSHI
Nipashe
Vitambulisho vya machinga vyamtoa ofisini

ZOEZI la ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga ambavyo vimechapishwa na Rais Dk. John Magufuli, kwa ajili ya kuwasaidia wasibughudhiwe wanapofanya biashara zao, limemsukuma Mkurugenzi mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Kastori Msigara, kutokaa ofisini.

Rais Dk. John Magufuli akionyesha kitambulisho cha wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga siku ya uzinduzi wa zoezi hilo.

Mkurugenzi huyo ameanza kazi ya kufanya ukaguzi wa ugawaji wa vitambulisho hivyo vya wajasiriamali wadogo, ikiwa ni siku chache baada ya kuripoti kazini, akitaka kupata uhalisia wa zoezi zima linavyoendelea.

Jana, Msigara alilazimika kutoingia ofisini na kwenda moja kwa moja katika Kata ya Mabogini kuongea na watumishi wa kata, kusikiliza kero za watumishi na wananchi wa eneo husika.

"Nimesema sikuja kushinda ofisini tu, nimekuja kufanya kazi na kazi yangu ya kwanza naanza nayo ni kufuatilia utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dk. John Pombe Magufuli ili kupata uhalisia wa zoezi zima," alisema.

Akizungumza na watumishi hao, Msigara alisema lengo la ziara hiyo pia ni pamoja na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya kata husika kwa kufuatilia, kusimamia, kuhakikisha kuna kuwapo na matumizi bora ya fedha za umma pamoja na kufanya ukaguzi wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo.

Katika mkutano huo, Msigara ameliwataka watendaji wa kata katika halmashauri hiyo kujitambua kuwa wao ndio wakurugenzi katika kata zao, hivyo wanawajibika kwa shughuli zote zinazotokea ndani ya kata.

Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, ina jumla ya kata 32, vijiji 157 na vitongoji 700 na ina majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Moshi Vijijini na Vunjo.

Habari Kubwa