Viwanda 30 vya dawa kujengwa

01Aug 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Viwanda 30 vya dawa kujengwa

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), inatarajia kuwa na viwanda 30 vya kutengeneza dawa na vifaa tiba nchini katika kutekeleza sera ya kukuza uchumi wa viwanda.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Adam Fimbo, alibainisha hayo juzi wakati wa kikao kazi na waandishi wa habari wa mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro kilichohusu usimamizi wa sheria ya dawa na vifaa tiba sura ya 19.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano, kumekuwa na ongezeko la wawekezaji wanaoomba kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini.

“Takwimu za nyuma zinaonyesha Tanzania inaingiza zaidi dawa na vifaa tiba kuliko zile zinazozalishwa nchini. Inaonekana asilimia 10 tu ya dawa na vifaa tiba ndiyo inazalishwa nchini, asilimia 90 tunaagiza, lakini hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2016,” alisema Fimbo.

Alisema uwekezaji katika sekta ya afya umekua na kwamba utafiti utakaofanyika tena, hali itakuwa tofauti kwa sababu hadi sasa nchini kuna viwanda 14 na viwanda 16 vipo katika hatua za mwisho kukamilika ujenzi ili kuanza uzalishaji.

Awali, akiwasilisha mada ya mchango wa TMDA katika kutekeleza sera ya viwanda, Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vifaa Tiba, Akida Khea, alisema wawekezaji wa ndani wamepata mwamko mkubwa katika uagizaji dawa.

“Kati ya wawekezaji 16 waliokuja kuomba kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba, ambaye si Mtanzania ni mmoja. Maana yake wawekezaji 15 ni Watanzania. Hii itatusaidia kukuza kipato cha nchi na kuongeza ajira,” alisema Khea.

Alisema wamehakikisha wawekezaji wanafuata taratibu zote za uanzishaji viwanda vya namna hiyo na wanawatembelea mara kwa mara ili kuhakikisha hawakiuki sheria.

Habari Kubwa