Viwanda vya mifuko ya hifadhi kuajiri 113,000

06Mar 2017
Daniel Mkate
Dar es Salaam
Nipashe
Viwanda vya mifuko ya hifadhi kuajiri 113,000

SHIRIKISHO ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini yenye mifuko sita, linatarajiwa kujenga viwanda 27 vitakavyotoa ajira kwa watu 113,000 baada ya kukamilika kwake.

Jenista Mhagama.

Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Eliud Sanga, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki baada ya kumalizika kwa kikao cha kupokea taarifa kufuatia agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Septemba 3, mwaka jana, kuitaka mifuko ya hifadhi kuwekeza kwenye viwanda.

Sanga akizungumza mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema katika utekelezaji huo, tayari shirikisho hilo limeanza maandalizi ya ujenzi wa kiwanda cha viua dudu kilichopo Kibaha pamoja na viwanda viwili vya sukari Mkulazi Ngerengere na Mbigiri vitakavyojengwa mkoani Morogoro.

Naye Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Meshack Bandawe, alisema viwanda vyote vitakapokamilisha ujenzi wake, vitaajiri wananchi wazawa 113,000.

Bandawe alisema ajira ya wananchi hao wazawa, itatokana na viwanda hivyo ambavyo baadhi yake vitajengwa na shirikisho la mifuko hiyo na vingine vitajengwa na mifuko ya hifadhi bila kutegemea ubia wa shirikisho.

Alitaja mifuko ambayo inaunda shirikisho hilo kuwa ni PPF, PSPF, LAPF, GEPF, NSSF na NIHF, iliyoungana kwa pamoja kutekeleza agizo la Rais Magufuli kujenga viwanda hadi ifikapo 2025.

Awali, Waziri Mhagama alisema ili nchi isonge mbele, lazima kuwapo na uwekezaji wenye tija badala ya ule wenye kuongeza matatizo.

“Kusiwapo na tatizo lolote ambalo litakwamisha katika uwekezaji, tija ni muhimu na manufaa kwa wawekezaji badala ya kuwawekea vikwazo…lazima mifuko ihakikishe inatatua vikwazo vinavyokwamisha sekta ya viwanda,” alisema Waziri Mhagama.

Aidha, alisema serikali ipo tayari kuondoa sheria na changamoto zote zinazokwamisha mifuko hiyo kushiriki kikamilifu katika sekta ya uendelezaji na ufufuaji viwanda.

Alisema azma ya serikali kuelekea nchi ya viwanda, hadi kufikia 2025 kuwapo na asilimia 75 ya lengo la mafanikio baada ya Watanzania milioni 20 kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Waziri Mhagama alisema kukutana kwa mifuko hiyo ya hifadhi mjini humu, inatokana na agizo la Rais Magufuli alilolitoa Septemba 3, mwaka jana jijini Arusha, ambalo alitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuwekeza katika viwanda.

Hata hivyo, Mhagama alisema ushiriki wa mifuko hiyo katika suala la kuwekeza katika nchi ya viwanda 2017-2021, linatekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Mifuko ya hifadhi ya jamii, ina jukumu kubwa sana katika utekelezaji wa agizo la Rais. Tumejiwekea malengo kufikia asilimia 75 hadi 2025, tuwe tumefanikiwa huku wananchi wetu zaidi ya milioni 20 wawe wamejiunga na mifuko ya sekta hiyo,” alisema.

Alisema iwapo mifuko hiyo itaanza utekelezaji wa agizo hilo la Magufuli, kutasaidia kuwapo kwa ongezeko kubwa la ajira kwa vijana wengi kupitia sekta ya viwanda.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliunga mkono utekelezaji wa agizo Rais linalofanywa na mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii, huku akiitaka iwe kipaumbele katika sekta hiyo.

Ummy alisema wizara yake itakuwa mnufaika mkubwa iwapo utekelezaji huo utakamilika kwa kupata dawa na vifaa tiba.

“Kwa sasa asilimia 85 ya vifaa, vifaa tiba pamoja na dawa zikiwamo panadol, zinanunuliwa nje ya nchi…katika bajeti ya wizara 2016/17 ya Sh. bilioni 200, fedha nyingi zinatumika kununulia vifaa nje badala ya kutumika kwa ajili ya matumizi mengine ya kiserikali kuweza kuwasaidia wananchi wake,” alisema Mwalimu.

Alisema iwapo viwanda vitajengwa nchini vikiwamo vya kuzalisha dawa na vifaa tiba, kutasaidia kupunguza gharama za kununulia vifaa nje ya nchi huku kiasi kingine cha fedha kikiingizwa katika sekta nyingine kwa ajili ya mahitaji kwa wananchi.

Hata hivyo, alisema kikwazo kitakachokuwapo ni ubora wa dawa na vifaa tiba, huku akiwataka watakaowekeza kwenye viwanda hivyo kuhakikisha wanazalisha vifaa na dawa zenye ubora na kiwango.

“Tusiuachie Mfuko wa Bima ya Afya (NIHF) pekee kuwekeza katika dawa na vifaa tiba, mifuko mingine mjichanganye ili kusaidiana na hao kwa lengo la kuzalisha dawa kwa wingi kutokana na kuwapo kwa soko la kutosha…kikubwa ubora na bei,” alisema.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, alisema iwapo mifuko hiyo itafanikisha kufufua kiwanda cha viatu kilichopo Gereza la Karanga wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kutasaidia taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kutoagiza nje ya nchi bidhaa hiyo.

Habari Kubwa