Viwanda vyahimizwa kutoa ajira za uhakika

07Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Viwanda vyahimizwa kutoa ajira za uhakika

WAMILIKI wa viwanda nchini wametakiwa kutoa ajira za uhakika na mikataba kwa wafanyakazi wao kutokana na asilimia kubwa ya viwanda nchini kuajiri wafanyakazi kama vibarua, jambo ambalo linatia shaka ajira zao.

Naibu Waziri Mifugo na Kilimo, Mary Mwanjelwa

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mary Mwanjelwa, alipotembelea kiwanda cha kusindika na kuchakata chai cha  Itona wilayani Mufindi mkoani Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili.

 

Mwanjelwa alisema kutoa ajira zisizo na mikataba na za vibarua ni sehemu ya kuwazalilisha wananchi umaskini kwani wanasalia kufanya kazi kubwa huku wakiishi kwa hofu.

 

 

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Itona Kata ya Ifwagi Mwanjelwa aliwahakikishia wakulima kuboreshwa soko la zao hilo kwa kutangaza bei elekezi ya serikali hivi karibuni ili kupunguza unyonyaji unaofanywa na wamiliki wa viwanda kwa kununua malighafi hizo kwa bei ya chini ambayo kwa kiasi kikubwa haiwanufaishi wakulima.

 

Aliwataka wamiliki wa kiwanda hicho kuongeza nguvu katika ununuzi wa chai kwa wakulima kwani asilimia 21 ya chai wanayonunua kwa wakulima wa zao hilo ni chache ukilinganisha na uzalishaji wao mkubwa.

 

Alisema wanapaswa kuongeza tija katika ununuzi angalau kufikia asilimia 40 ili kuwaongezea soko wakulima hao, jambo litakalowanufaisha ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji ukilinganisha na uzalishaji.

 

Pia aliwataka kuanzisha mashamba darasa kwa ajili ya kutoa elimu ya kilimo bora cha chai kwa wakulima hao ili wazalishe chai bora.

 

Katika hatua nyingine, Mwanjelwa aliwapongeza wamiliki wa kiwanda hicho kwa kuajiri idadi kubwa ya Watanzania kutokana na takribani 1,500 wameajiriwa huku wageni wakiwa wanne tu.

 

Mwanjelwa alihitimisha ziara ya kikazi mkoani Iringa ambapo alitembelea pia kiwanda cha kuchakata pareto cha PCT mjini Mafinga na kukagua maabara ya kupima ubora wa pareto sambamba na kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho ili kuboresha na kuongeza bei ya ununuzi wa zao hilo kwa wakulima.

 

Habari Kubwa