Vodacom Foundation yaipiga jeki hospitali

17Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Masasi
Nipashe
Vodacom Foundation yaipiga jeki hospitali

HOSPITALI ya Mkomaindo wilayani Masasi, mkoani Mtwara, itaondokana au kupunguza vifo vya watoto wachanga vitokanavyo na changamoto mbalimbali, baada ya kukabidhiwa msaada wa vifaa tiba kutoka Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation.

Waziri wa Uwekezaji, Geoffrey Mwambe (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Claudia Kitta (kulia), wakipokea baadhi ya vifaa tiba kutoka kwa Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia, kwa ajili ya kusaidia utoaji huduma za matibabu kwa watoto njiti katika Hospitali ya Mkomaindo, wilayani humo, mkoani Mtwara juzi. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Pia, watoto njiti katika hospitali hiyo wataondokana na changamoto ya kukaa wawili katika mashine maalumu (incubator), baada ya kusaidiwa nyingine na taasisi hiyo.

Wakikabidhiwa vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh. milioni 67, jana, Kaimu Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Masasi, Dk. Amina Moshi, alisema vifaa tiba hivyo vimelenga kitengo cha uzazi kwa mama na watoto wachanga, hivyo vitasaidia kuboresha huduma za afya.

“Tulikuwa na changamoto ya vifaa tiba vinavyoweza kusaidia watoto wachanga kupata joto baada ya kuzaliwa na incubator kwa ajili ya watoto njiti waliozaliwa kabla ya kutimiza miezi tisa… vifaa vingine kama mashine za oksijeni vitawasaidia katika kupumua kwa wale wenye tatizo la kupumua baada ya kuzaliwa,” alisema Dk. Amina.

Alibainisha halmashauri hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya vifo vya watoto wachanga ambapo Januari hadi Desemba 2020 kulikuwa na vifo vya watoto wachanga 165 na Januari hadi Julai 2021 kumekuwa na vifo 63.

Alisema kwa upande wa vifo vya kinamama Januari hadi Desemba 2020 vifo vitokanavyo na uzazi vilikuwa 10 na Januari hadi Julai 2021 vilikuwa vifo sita hivyo msaada huo wa vifaa tiba vitasaidia sana kupunguza vifo hivyo.

Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia, alisema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na serikali katika maeneo mbalimbali kama afya na kilimo ili kugusa jamii hususani katika afya ya uzazi.

Alisema wamekuwa wakifanya uhamasishaji na kampeni mbalimbali kwa kutumia mtandao wa simu kwa kutuma ujumbe mfupi pamoja na njia nyingine za mawasiliano ili kupeleka taarifa mbalimbali za afya kama tatizo la fistula.