W’biashara sasa kupata mkopo CRDB wa kutoa mizigo bandarini

28Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
W’biashara sasa kupata mkopo CRDB wa kutoa mizigo bandarini

BENKI ya CRDB imesaini mkataba wa makubaliano na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) kuwezesha kulipia gharama za kutoa mzigo bandarini.

Ofisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Dk. Joseph Witts (wa pili kushoto), akibadilishana mkataba na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini (JWT), Mchungaji Silva Kiondo, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kutiliana sahihi mkataba wa makubaliano utakaowawezesha wafanyabiashara kupata mkopo wa kulipa gharama za kutoa mizigo bandarani kwa riba nafuu. Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara cha Benki hiyo, Toyi Ruvumbangu (kushoto) na Mkurugenzi wa Mawasiliano JWT, Stephen Chamle. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini, Ofisa Mkuu wa Biashara wa CRDB, Dk. Joseph Witts, alisema ushirikiano huo utawawezesha wafanyabiashara kulipia gharama za kutoa mizigo bandarini kwa mkopo (Post Import Financing Solution) na kuondokana na changamoto za ucheleweshaji wa mizigo ambazo huongeza gharama.

Dk. Witts alisema huduma hiyo ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Benki ya CRDB kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara nchini.

Alisema ili kutoa unafuu zaidi kwa wafanyabiashara, benki hiyo imepunguza riba katika huduma hiyo na wateja watakuwa wakitozwa asilimia 16 kulinganisha na asilimia 18 inayotozwa katika mikopo ya kawaida.

Katika makubaliano hayo CRDB itakuwa ikisaidia kulipa gharama za kutoa mizigo bandarini na wafanyabiashara kulipa katika kipindi cha miezi mitatu.

Akielezea taratibu za upatikanaji wa huduma hiyo, Dk. Witts alisema huduma hiyo itatolewa kwa wafanyabiashara ambao ni wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania.

“Mkopo huu hutolewa kulingana na kiwango cha gharama za malipo ya mzigo uliopo bandarini ambapo mfanyabiashara anaweza kulipia gharama za kodi ya forodha, gharama za bandari na wakala wa meli kwa wakati na bila kuchelewa,”
aliongezea Dk. Witts na kufafanua kuwa riba hiyo inaweza kupungua zaidi kutokana na mwitikio na uaminifu utakao kuwa ukionyeshwa na wafanyabiashara.

Mkopo huo wa gharama za tozo/ kodi ya mizigo iliyoagizwa kutoka nje inatolewa kwa masharti nafuu bila ulazima wa kuwa na dhamana ya mali isiyohamishika na hutolewa kwa riba nafuu na mteja atapata fedha kwa muda mfupi usiozidi siku saba atakapowasilisha ombi la mkopo.

Aidha, malipo ya kodi na gharama za kodi na bandari zitalipwa moja kwa moja kwenye taasisi husika ikiwamo TRA, TPA au Wakala wa meli. Dk. Witts alisema wamefanya hivyo ili kusaidia na kurahisisha ulipaji kodi kwa wakati.

“Dhumuni letu ni kuleta urahisi kwa wafanyabiashara kupata bidhaa/ mizigo yao pindi wanapoagiza kutoka nje. Vilevile huduma hii itasaidia jitihada za serikali kukusanya kodi kwa wakati na kuboresha uchumi wa nchi kwa kuhakikisha wafanyabiashara wote wanalipa kodi katika muda uliowekwa kama ambavyo serikali imekua ikisisitiza,” alisema Dk. Witts.

Alisema huduma hiyo itatoa nafuu kwa wafanyabiashara kipindi hiki cha corona wakati biashara nyingi zimepata changamoto.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Mchungaji Silva Kiondo aliishukuru Benki ya CRDB kwa kutambua umuhimu wa wafanyabiashara kupitia jumuiya hiyo na kubuni huduma hiyo ambayo itakwenda kuondoa changamoto nyingi wakati wa uingizaji wa bidhaa nchini.

“Tunajivunia kwa Jumuiya yetu kufikia mafanikio haya, malengo yetu ni kuona wanachama wetu wanafanya biashara zao bila usumbufu wa aina yoyote. Nitoe wito sasa kwa wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa nje kutumia fursa hii kuboresha biashara zao,” alisema Mchungaji Kiondo huku akisema jumuiya hiyo imejipanga kukamilisha na kuhakikisha inawahudumia kikamilifu wafanyabiashara ili wawe na uhakika na biashara zao.

Habari Kubwa