W’biashara wa soko wamwomba RC

01Jul 2020
Peter Mkwavila
Dodoma
Nipashe
W’biashara wa soko wamwomba RC

WAFANYABIASHARA zaidi ya 100 wa matunda katika soko la Sabasaba jijini hapa, wamemwomba Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Bilinith Mahenge, kuangalia suala la ushushaji wa mizigo ili kuwapunguzia gharama kutokana na sasa mizigo yote ikitakiwa kushukia soko jipya la Job Ndugai.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Bilinith Mahenge:PICHA NA MTANDAO

Walisema hayo jana wakati wa mkutano wao ambao pia ulihudhuriwa na Ofisa Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Michael Ngoi, alisema wamekuwa wakiingia gharama kubwa kusafirisha mikungu ya ndizi.

“Kulitolewa tangazo kuwa magari yote makubwa na madogo yashushie mizigo Nanenane kwenye sojo jipya, jambo hili linatugharimu sana tunawaza baada ya miezi mitatu mitaji itakuwa imekata kabisa,’’alisema.

Alisema kabla ya kutolewa kwa agizo hilo, mizigo ilikuwaikishushiwa viwanja vya barafu na gharama ya kusafirisha mkungu moja mpaka sokoni ilikuwa ni Sh. 700 lakini sasa gharama ya kusafirisha mkungu moja wa ndizi ni Sh. 2,600.

“Mzigo ukishukia soko jipya ukitaka kusafirisha kwenda soko laSabasaba gharama ni kubwa, kushusha kila mkungu ni Sh. 200, kubeba Sh. 200, kupakia Sh. 1,500, ukifika sokoni kushusha na kupeleka ndani ni Sh. 400 na hiyo ni gharama ya mkungu moja tu wa ndizi.

Mfanyabiashara mwingine, Matanza Matanza, alisema waliwahi kupeleka malalamiko kwa mkuu wa mkoa, lakini mpaka sasa hajajibiwa.

 

Ofisa Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna, alisema suala la kushusha mizigo soko la Ndugai lilitolewa na Mkuu wa mkoa, Dk. Mahenge.

“Pale mfanyabiashara anapokuwa na hoja anasikilizwa, mkuu wa mkoa wakati anasema hayo alikuwa na nia njema tu, kuna wafanyabiashara soko jipya kwa hiyo mizigo ikishushwa pale wafanyabiashara wa pale wawewananuanua mizigo soko la jumla na kupanga kwenye vizimba vyao,” alisema.

Alisema hoja zao amezichukua na zitafikishwa mamlaka husika. “Hoja zenu nitazifikisha mamlaka husika na mtapatiwa majibu,” alisema

Habari Kubwa