Waajiri wasiojisajili fidia waonywa

06Jul 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Waajiri wasiojisajili fidia waonywa

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi(WCF), umewaomba waajiri ambao bado hawajajisajili na mfuko huo kufanya hivyo ili kuwasaidia wafanyakazi wao kupata fidia wanapopatwa na matatizo kazini.

Wito huo ulitolewa  jana na Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini wa WCF, Dk. Abdulssalam Omary, katika Maonyesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DTIF) yanayofanyika jijini Dar es Salaam

Dk. Omary alisema lengo la mfuko huo ni kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta rasmi ya umma na binafsi Tanzania Bara ambao hupata matatizo ya kuumia, kuugua au kufariki dunia kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba yao. 

Alisema asilimia 85 ya waajiri wakubwa wamejisajiri na  mfuko huo, huku waajiri wadogo waliojisajiri wakiwa 75 na kwamba ni vyema kwa waajiri ambao hawajajisajili wakafanya hivyo haraka.

Alisema mfuko huo ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoundwa kwa mujibu wa sheria kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263 marejeo ya mwaka 2015 na kwamba kujisajili ni muhimu

"Mfanyakazi atakapoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi,  WCF utatoa huduma za matibabu, malipo ya ulemavu, malipo ya ulemavu wa kudumu, malipo ya anayehudumia mgonjwa, huduma za ukarabati na ushauri nasaha, msaada wa mazishi na malipo ya wategemezi," alisema.

Dk. Omary alisema tangu mwaka 2016 mpaka 2018,  jumla ya Sh. bilioni sita zimelipwa kwa wafanyakazi waliopatwa na matatizo wakiwa kazini.

"Ninatoa wito pia kwa wafanyakazi kufuatilia kwa ajili ya kubaini kama waajiri wao wamejisajili na mfuko huu kwa sababu ni muhimu sana kwao, " alisema.

Habari Kubwa