Waanza tahadhari kunusuru mifugo dhidi ya magonjwa

10Jun 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Waanza tahadhari kunusuru mifugo dhidi ya magonjwa

WANANCHI wa Kata ya Uru Kusini katika Jimbo la Moshi Vijijini, wameanza kuchukua tahadhari ya kuikinga mifugo yao na maambukizi ya ugonjwa kimeta kwa kuchanja mifugo 3,856.

Diwani wa Kata hiyo, Wakili Wilhard Kitali, alieleza kuwa wameanza uhamasishaji wa juu ya umuhimu wa kuchanja mifugo kuzuia magonjwa mbalimbali.

Alikuwa akitoa taarifa kuhusu zoezi hilo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kilichofanyika siku chache zilizopita.

"Ni kweli tumeshachanja ng'ombe 1,768, kondoo na mbuzi 1,567 na nguruwe 521 kwa ajili ya kuzuia magonjwa mbalimbali ikiwamo kimeta na zoezi bado linaendelea," alisema.

Aidha, uongozi wa kata hiyo umesema kazi nyingine zinazofanyika kwa umakini mkubwa ni pamoja na ukaguzi wa nyama na kukusanya ushuru wa ukaguzi.

Diwani Kitali alisema pia kuwa wafugaji 725 wanaendelea kupewa elimu juu ya ufugaji, kuchanja mifugo na kuotesha malisho.

"Yapo mambo ambayo tunadhani ni muhimu wananchi wa eneo hili wakapata mwanga wa elimu kwa mfano elimu juu ukamuaji wa maziwa na usindikaji," alisisitiza Kitali.

Kata ya Uru Kusini inaundwa na vijiji saba na vitongoji 20 vyenye kaya 5,926 zenye idadi ya watu 22,904.

Habari Kubwa