Waathirika wanyamapori wadai vifuta jasho 828m/-

12May 2018
Augusta Njoji
  Dodoma
Nipashe
Waathirika wanyamapori wadai vifuta jasho 828m/-

JUMLA ya Sh. milioni 828 zinadaiwa kama vifuta jasho kwa wananchi waliopata madhara yanayotokana na uharibifu wa wanyamapori, Bunge lilielezwa jana mjini hapa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, alisema alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Namtumbo (CCM), Edwin Ngonyani, aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kutoa vifuta jasho kwa wananchi walioathirika na maafa ya wanyamapori katika kata ya Likuyu Sekamaganga na ambao walishafanyiwa tathmini.

Akijibu swali hilo, Hasunga alisema matukio ya wanyama waharibifu ni mengi sana nchini na yanatokana na kuongezeka kwa wanyama.

“Hivi sasa kuna matukio zaidi ya 3510 wananchi wameathirika kutokana na wanyama waharibifu na jumla ya fedha hadi sasa zinazodaiwa ni Sh. milioni 828 katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema.

Alisema hivi sasa serikali inatafuta fedha ili kuhakikisha wananchi walioathirika na wanyamapori wanapata kifuta jasho na  fedha zitakapopatikana zitalipwa mara moja.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainab Vullu alitaka kujua serikali imejipangaje kutoa pilipili nyingi ili kudhibiti tembo.

Naibu Waziri Hasunga alisema wamehamasisha wananchi wa maeneo yaliyo jirani na hifadhi kulima pilipili kwa wingi.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alitaka kujua serikali ina mpango gani juu ya wanyamapori waharibifu hususan tembo ambao wamesambaa ovyo katika jimbo hilo na kufanya uharibifu mkubwa pamoja na kuua watu.

“Je, ni lini serikali itaruhusu vijiji kumiliki silaha kwa ajili ya kujilinda na wanyama hao wakali na je, tembo wana thamani kubwa kushinda uhai wa watu?”Alihoji.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Hasunga alisema suala la wanyamapori wakali na waharibifu limekuwa likijitokeza kwenye zaidi ya wilaya 80 nchini.

Hata hivyo, alisema ongezeko la watu limesababisha kuzibwa kwa shoroba za wanyamapori pamoja na maeneo ya mazalia na matawanyiko yao.

“Kuzibwa kwa shoroba hizi kumeongeza migongano baina ya binadamu na wanyamapori. Ili kukabiliana na hili serikali itaendelea kufanya doria za kudhibiti wanyamapori,” alisema.

Aidha alisema kwa mwaka 2017/18 Wizara hiyo imelipa Sh. milioni 7.5 kwa wananchi 27 wa wilaya hiyo walioathiriwa na wanyamapori.

Alisema suala la utoaji silaha litaangaliwa pale watakapokuwa wakipitia sheria na kwamba kuhusu vifuta jasho vinatolewa kwa mujibu wa kanuni za kifuta jasho na machozi za mwaka 2011 na  mtu aliyeuawa ni Sh. milioni moja na aliyejeruhiwa ni Sh. 500,000.