Wabunge wasikitishwa uchakavu nyumba NHC

18May 2022
Romana Mallya
DODOMA
Nipashe
Wabunge wasikitishwa uchakavu nyumba NHC

WABUNGE wameonyesha kusikitishwa na nyumba zinazomilikiwa na Shirika la Nyumba Nchini (NHC) katika miji ambazo wamesema nyingi zimechakaa.

Katika semina ya wabunge iliyofanyika juzi iliyoandaliwa na NHC, wabunge hao walisema uchakavu huo umesababisha kutopendeza kwa maeneo hayo.

Mbunge wa Chakechake (CCM), Ramadhan Suleiman Ramadhan alisema nyumba nyingi zilizojengwa katika miji hazifanyiwi maboresho na hivyo hazifai tena katika miji.

"Matajiri nikiwamo ninaweza kujenga nyie mkapata faida na mimi nikapata faida,”alisema.

Mbunge wa Geita Mjini (CCM) Constatine Kanyasu alisema gharama kubwa za kujenga zinasababisha bei ya kupangisha nyumba za shirika hilo kuwa kubwa na kusababisha baadhi kuhama.

"Baadhi ya wapangaji tumehama Medelii kwa sababu bei ya kupangisha ni kubwa ukilinganisha na huko uraiani,”alibainisha.

Akieleza suala la uchakavu wa nyumba hizo kwenye miji, Mkurugenzi Mtendaji wa NHC, Nehemia Mchechu alisema kwa kufuata utaratibu itawachukua muda mrefu kukarabati ndiyo maana wameamua kwenda katika utaratibu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma (PPP).

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Allan Kijazi, alisema jambo la msingi ni kupata miongozo kwa mji wa Dodoma hasa kwa kuzingati una matetemeko ya ardhi.

Alisema ujenzi hufanyika kama ardhi inafaa kwa ujenzi.

"Kuna wakati mji wa Serikali (Mtumba) ilitokea matetemeko mawili, matatu lakini kuna baadhi ya majengo ya ofisi tayari yameshaathirika na matetemeko haya, baada ya uchunguzi kufanyika na kuonyesha kuwa kuna baadhi ya maeneo hayafai kwa ujenzi, ilibainishwa kuwa maeneo ambayo yana matatizo na hivyo yasiwe yanajengwa majengo yoyote," alisema.

Alisema kabla ya ujenzi serikali imekuwa ikizingatia kuchunguza eneo husika.

Akizungumzia miongozo ya ujenzi, Dk Kijaji alisema wako katika hatua za mwisho za kuandaa sera za nyumba na zikikamilika kutakuwa na miongozo kamili ya ujenzi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula alisema wakitaka kujenga nyumba yoyote katika halmashauri wamekuwa wakiangalia takwa (taste) ya mteja na ukubwa wa nyumba anayohitaji.

Kuhusu kuingia makubaliano na halmashauri ili waweze kununua majengo, Dk. Mabula alisema kuna halmashauri ziliingia makubaliano na NHC lakini mwisho wa siku waliingia katika mvutano wa kuchukua ama wasichukue nyumba hizo.

Habari Kubwa