Wabunge watolewa hofu mafuriko SGR

03Dec 2018
Mary Geofrey
kilosa
Nipashe
Wabunge watolewa hofu mafuriko SGR

WABUNGE wa kundi la maendeleo endelevu, wametolewa shaka kuhusu mradi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), inayojengwa karibu na eneo la mto Mkondoa kuwa haitaingiliwa na mafuriko.

Meneja Mradi huo wa kipande cha pili kuanzia Morogoro-Makutopora, Mhandisi Faustine Karaia, aliwatoa wasiwasi wabunge hao waliokuwa wakikagua mradi huo kutoka Dar es Salaam hadi Kilosa na kusema reli hiyo itapita juu na katikati ya milima ili kukwepa uharibifu wa matumizi ya mto huo.

 

Mhandisi Karaia alisema reli hiyo imejengwa umbali mrefu kutoka ulipo mto huo, lakini wamepitisha maeneo ya reli ili kukwepa kulipa fidia kubwa kwenye maeneo ya wananchi.

 

Aidha, alisema reli ya awali imeingiliwa na shughuli za mto kwa sababu ilijengwa kwa teknolojia ya chini, lakini pia matumizi ya mto huo yameongezeka tofauti na awali.

 

Alisema maji hayo yanatoka maeneo mbalimbali ndio sababu yanasababisha madhara kwenye reli ya zamani.

 

“Teknolojia ya reli ya zamani ni ya mwaka 1880 na ilikuwa ni ya kufuata mikondo ya maji na milima, na hatuwezi kulaumu, lakini teknolojia ya sasa tunayo ya kupasua milima na kupitisha reli," alisisitiza.

 

Alieleza zaidi kuwa reli hiyo inajengwa kwa kiwango cha kudumu miaka 100 na kwamba kinachotakiwa ni kutunza mazingira ili kuondokana na uharibifu huo.

 

Awali wabunge hao, walieleza wasiwasi kuwa kama itaweza kuhimili maji ya mto Mkondoa ambao umekuwa ukisababisha maafa makubwa na kusababisha safari za treni kusimama.

 

Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, alitaka kufahamu kutoka kwa wahandisi wa mradi huo, kama mto huo hautakuwa na madhara kwa reli hiyo ya kisasa.

 

Alisema mto huo umekuwa ukisababisha madhara kwa reli ya zamani na kusababisha maafa kwa watumiaji wake.

 

Alisema reli ya zamani ilikuwa na matuta, lakini mikondo ya maji iliongezeka na kuingilia reli na maji na kusababisha kuchakaa kwa miundombinu.

 

 

 

 

 

 

Habari Kubwa