Wabuni mbinu kuficha bidhaa feki

25Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Kigoma
Nipashe
Wabuni mbinu kuficha bidhaa feki

BAADHI ya wafanyabiashara wamebuni mbinu mpya ya kuficha bidhaa, ambazo zimepigwa marufuku katika Soko la Tanzania hasa vipodozi kama hatua ya kukwepa ukaguzi wa serikali.

Hayo yalisemwa jana na Ofisa Usalama wa Chakula wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Elisha Meshack wakati wa ukaguzi uliofanyika, mkoani Kigoma.

Alisema ukaguzi huo umefanyika kwenye maduka ya rejareja, jumla, kwa wasambazaji, maduka makubwa, migahawa na kwingineko, pia wametoa elimu kwa wananchi.

Ofisa huyo alisema wamebaini mbinu hizo, kwenye ukaguzi wa bidhaa sokoni katika Wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko, mkoani Kigoma kwa lengo la kuhakikisha bidhaa zote zinazouzwa sokoni zinakidhi matakwa ya kiwango husika.

Alisema kuna wafanyabiashara wachache wasio waaminifu wanaoficha bidhaa zilizopigwa marufuku kwenye Soko la Tanzania hasa vipodozi kwenye mabegi yao ya mkononi au katika ndoo za kuwekea uchafu dukani na endapo mteja anatokea basi anapatiwa bidhaa hiyo kwa kificho.

Meshack alifafanua kuwa TBS haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wote watakaobainika kuuza bidhaa zilizopigwa marufuku, kwani ni kinyume cha sheria.

Alisema kwa kuwa mbinu wanazozitumia tayari zimebainika, shirika hilo litahakikisha wafanyabiashara wachache wadanganyifu, ambao wanauza bidhaa za vipodozi vilivyopigwa marufuku kwa kificho wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Ukaguzi huo, alisema  ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo, kusimamia vyema majukumu yake kwa kuhakikisha ubora wa bidhaa na kulinda afya na usalama wa Watanzania na watumiaji wote.

Wakizungumzia ukaguzi huo, wananchi wengi waliunga mkono hatua hiyo ya TBS ya kufanya ukaguzi na kutoa elimu kwa umma, kwa kuwa kitendo cha wafanyabiashara kuuza kwa kificho bidhaa zilizopigwa marufuku ni kielelezo, kuwa elimu imewafikia na wanajua kwamba wanavunja sheria.

"Tunafurahishwa na kazi inayofanywa na TBS kwani hata watumiaji wa bidhaa za vipodozi sasa hivi wanajua ni vya aina gani havitakiwi kwenye Soko la Tanzania. Tunawapongeza  kwa kazi kubwa," alisema Joyce Edward, mkazi wa Kibondo.

Alisema ukaguzi huo utakuwa mwarobaini wa wafanyabiashara, ambao wamekuwa wakiuza bidhaa za chakula na vipodozi zilizokwisha muda wa matumizi na vilevile kuuziwa vipodozi vyenye viambata sumu.

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Naftary Elisha, alisema; “Naishukuru TBS kwa kufika kwetu kwani kwa kufanya hivi. Ninaamini  sisi wananchi tutaepukana na udanganyifu wa wauzaji sababu wanachukulia udhaifu wetu wa kutojua mambo au kutosoma na kutuuzia bidhaa, ambazo hazina ubora na zilizokwisha muda wa matumizi. Nashauri jambo hili hili liwe endelevu, ili tabia hii ya udanganyifu kwa wananchi ikome kabisa,” alisema.

Habari Kubwa