Wabuni mbinu mpya ya kuwaibia wakulima

18Mar 2019
Elisante John
SINGIDA
Nipashe
Wabuni mbinu mpya ya kuwaibia wakulima

BAADA ya serikali kupiga marufuku ujazo wa lumbesa katika ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima, baadhi ya wafanyabiashara wamehamishia biashara zao mashambani.

Badala ya kununua vitunguu kwenye Soko la Kimataifa la Misuna lililoko Manispaa ya Singida, wafanyabiashara hao sasa wanawafuata wakulima mashambani na kupima vitunguu kwa kutumia magunia yenye ujazo mkubwa.

Wafanyabiashara hao kutoka ndani na nje ya nchi, wanadaiwa kuwanyonya wakulima kupitia magunia maarufu kwa jina la Tshishimbi, ambayo zimepigwa marufuku na uongozi wa halmashauri kutokana na kuwa na ujazo wa zaidi ya Kg 100.

Kutokana na changamoto hiyo, wakulima wameiomba serikali iwafuatilie wafanyabiashara hao vijijini ili wakulima wanufaike na mazao yao.

Mwenyekiti wa Soko la Misuna, Abdalarahaman Mbogo, alisema wafanyabiashara hao baada ya kudhibitiwa, walichukua magunia hayo na kwenda nayo vijijini ambako wamekuwa wakiyatumia kuwaibia wakulima.

“Tunaomba serikali ya mkoa kushirikiana na wenzao wa vijijini na mikoa mingine inayolima zao hili kupiga vita magunia hayo ya nyavu yanayobeba vitunguu zaidi ya Kg 100," alisema.

“Pia, kuna ujanja wa kutumia ndoo kubwa zilizotanuliwa kwa lengo la kumnyonya mkulima kule kule vijijini. Mbaya zaidi, wanapopima kwa ndoo, inabidi mpime ndoo sita ndipo eti wanahesabu gunia moja, jambo hili siyo sawa, wanawanyonya wakulima."

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskas Muragili, alikemea matumizi ya vipimo hivyo katika ununuzi wa vitunguu na mazao mengine ya wakulima na kuagiza viongozi wote kushirikiana kuwadhibiti wahusika.

Alisema serikali itaendelea na jitihada ya kulinda mazao ya wakulima ili wasiendelee kunyonywa.

Habari Kubwa