Wachimbaji sasa waomba vifaa vya kinga

10Oct 2019
Grace Mwakalinga
Songwe
Nipashe
Wachimbaji sasa waomba vifaa vya kinga

WACHIMBAJI wadogo wa madini katika Mji wa Mkwajuni, Halmashauri ya Wilaya Songwe wameiomba serikali kusaidia upatikanaji wa vifaa kinga ambavyo vitawasaidia kuwakinga dhidi ya athari zinazotokea kwenye shughuli za uchimbaji dhahabu.

Walitoa ombi hilo juzi, walipozungumza na Nipashe ambapo walidai wanafanya kazi kwenye mazingira magumu na hatari kwa afya yao kwa sababu vifaa vya uchimbaji wanavyovitumia ni hatari.

Walisema licha ya kuwa wanatambua matumizi ya zana holela kwenye shughuli za uchimbaji dhahabu yana madhara, hivyo wameshindwa kumudu gharama za kununulia mashine za kisasa kwa ajili ya uchimbaji.

Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini Mkoa wa Songwe, Emmanuel Kamaka, alisema matumizi ya zebaki katika shughuli za uchimbaji madini ni hatari kwa afya zao, hivyo uwapo wa vifaa kinga utasaidia kupunguza madhara yanayopatikana.

“Tunaomba serikali itusaidia vifaa kinga katika shughuli zetu za uchimbaji kama itashindwa kutununulia basi watusaidie kutafuta wakala ambaye atakuja hapa mkwajuni kutuuzia tupo tayari,” alisema Kamaka.

Mbali na kuiomba serikali kuwanunulia vifaa tiba, pia alieleza kufurahishwa na mafunzo ya afya na usalama kwenye maeneo yao ya migodi ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha).

Alisema mafunzo hayo yamewasaidia kujifunza masuala mbalimbali ya kujilinda na kukabiliana na athari zinazotokea wakati wa shughuli za uchimbaji wa dhahabu.

Alisema wachimbaji hao hawajawahi kupata mafunzo yoyote ya usalama na afya katika migodi yao, hivyo aliipongeza Osha kwa kuandaa utaratibu huo na kuwaomba kuwatembelea mara kwa mara kutoa elimu hiyo ambayo ina manufaa kwao.

Mwanaidi Sembo alieleza wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu hususani wanawake wanavyokabiliwa na changamoto ya vifaa.

Alisema vifaa vinavyotumika kwenye shughuli za uchimbaji kama kole na sululu sio rafiki kwao na kuiomba serikali kuandaa utaratibu mwingine wa namna ya kuwapatia vifaa vizuri ambavyo vitarahisisha shughuli za uchimbaji.

Meneja Afya Osha, Jerome Materu, katika mafunzo hayo alitoa tahadhari kwa wachimbaji hao kuachana na matumizi ya zebaki kwani ni hatari kwa afya zao.

Materu alisema vitu hivyo vinasababisha madhara makubwa kwenye mwili wa binadamu ikiwamo vilema vya miguu na mikono, hivyo kushindwa kutembelea na kurithisha kizazi chake.

“Matumizi ya zebaki ni hatari kwa afya, hivyo nawasihi wachimbaji mwachane na vitu hivyo tafuteni teknolojia nyingine ya kupata madini hata kama ni bei ghali, lakini bora kununua ili kuokoa maisha yako na kizazi chako,” alisema Materu.

Habari Kubwa