Wachimbaji tanzanite wapatiwa elimu ugonjwa wa upumuaji

15Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Mirerani
Nipashe
Wachimbaji tanzanite wapatiwa elimu ugonjwa wa upumuaji

WACHIMBAJI wadogo 13,328 wa madini ya tanzanite katika migodi ya Mirerani, wamepata elimu ya kujikinga na kifua kikuu, Ukimwi na ugonjwa unaosababisha tatizo la upumuaji (silicosis).

Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (Mkuta), Thobias Magati, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumzia kazi za huduma ya jamii kwa mwaka jana.

Alisema katika watu hao 13,328 waliofikiwa, wanaume walikuwa 11,307, wanawake 1,804 na watoto ni 217 na wagonjwa waliogundulika ni 123.

Alisema kwa kushirikiana na Hospitali ya Kibong’oto OHSC ambayo ni maalum kwa ajili ya magonjwa ya kifua kikuu iliopo wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjro, waliweza kufanikiwa kutoa huduma hiyo.

"Uwezeshaji ndiyo mdogo ila tumeweza kufungua matawi ya Mkuta kwenye maeneo ya kitalu B (Opec) na kitalu D ambayo yapo kwenye migodi inayowazunguka ili kusaidia shughuli za uibuaji," alisema.

Alisema wanafanya hayo ili kufikia malengo ya tamko la kisiasa la umoja wa mataifa la kutokomeza kifua kikuu ifikapo mwaka 2022.

Katibu wa Mkuta, Benjamin Kaba, alisema wanakabiliwa na changamoto ya wagonjwa wengi wa kifua kikuu, gharama ya ufuatiliaji na kutopata vipimo kwa wakati.

Alisema changamoto nyingine ni wachimbaji wengi wanaugua ugonjwa wa silicosis na pneumonia ambayo yanahitaji kufanyiwa utafiti wa kina zaidi na mabadiliko ya ukuta yamesababisha wagonjwa kushindwa kutoka kwenda kupata huduma.

Alisema changamoto nyingine ni kuhamahama kwa wagonjwa kwenda migodi mingine ya Kitwai, Lemshuku, Mwajanga, Landanai na Kimwengani.

Alisema wana mikakati mingi yakufanikisha mipango yao ila wanakwamishwa kutokana na ukata unaowakabili kwa kuwa hawana mfadhili wa kukisaidia kikundi hicho chenye wanachama 58.

Mjumbe wa Mkuta, Mwasiti Ntandu, alitoa wito kwa serikali kuiangalia Mirerani kwa jicho la pekee kwa kuwa magonjwa ya kifua kikuu na silicosis inayosababishwa na ulanga imewaathiri watu wengi.

Alisema baadhi ya wachimbaji wamewaacha wajane na yatima kutokana na kuugua maradhi hayo ambayo yanaweza kutibika.

Habari Kubwa