Wachimbaji wa Tanzanite watakiwa tahadhari corona

20Mar 2020
Allan lsack
Simanjiro
Nipashe
Wachimbaji wa Tanzanite watakiwa tahadhari corona

WACHIMBAJI wa madini wa Mkoa wa Manyara, wametakiwa kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa corona.

Wametakiwa kufuata maagizo ya serikali ya kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono kila mara kwa maji yanayotiririka na kuvaa barakoa hata nje ya migodi yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini mkoani Manyara (Marema), Justin Nyari, aliyasema hayo wakati akizungumzia mikakati ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa corona kwa wachimbaji madini wa eneo hilo.

Nyari alisema wachimbaji hawanabudi kuchukua tahadhari ya maambukizi ya ugonjwa huo, kwa kutimiza maagizo ya serikali yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Alisema japokuwa wachimbaji madini wanavaa vifaa vya barakoa kujikinga na vumbi na hewa chafu wakiwa ndani ya mgodi, lakini kwa sasa wanapaswa kuvaa hata nje ya migodi.

Pia alisema tahadhari za afya zinapaswa kuchukuliwa kwa maeneo ya machimbo ukiwamo usafi kwa wachimbaji kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kwenye maeneo yote migodini na kwenye migahawa.

"Kama tukiona kuna mtu mwenye dalili za mafua makali, kuumwa kichwani, kushindwa kupumua, tunaomba tutoe taarifa kwa mamlaka husika kwenye eneo la jirani," alisema.

Alisema maagizo ya serikali ya kunawa kila mara yanapaswa kutekelezwa kwenye kila mgodi kuweka maji na sabuni mlangoni ili watu wote wanaoingia na wanaotoka migodini kunawa mikono kila wakati.

Mmoja wa wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, Hassan Juma, alisema wachimbaji wanapaswa kuchukua tahadhari zinazotolewa na viongozi wa serikali.

Alisema hadi sasa hakuna taarifa ya mchimbaji madini kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, lakini wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa.

"Hatupaswi kusubiri mtu mwenye corona aonekane migodini na serikali ifunge migodi, tuchukue tahadhari ili ugonjwa usiingie, na serikali isisitishe uchimbaji kwa kuwa tutakufa njaa, tuwe makini tusiruhusu maambukizi kwenye uchimbaji," alisema.

Habari Kubwa