Wachimbaji walalamikia gharama kubwa za vibali

29Jul 2021
Grace Mwakalinga
Chunya
Nipashe
Wachimbaji walalamikia gharama kubwa za vibali

WACHIMBAJI wa madini katika Wilaya ya Chunya, wamelalamikia gharama kubwa ya upatikanaji wa vibali vya matumizi ya vilipuzi, wakidai hulazimika kufuata huduma hiyo jijini Dodoma na kuwagharimu fedha nyingi.

Kutokana na adha ya kusafiri hadi jijini Dodoma kufuata kibali kwa ajili ya matumizi ya vilipuzi maarufu kama baruti kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini wilayani Chunya, wameiomba serikali kuwasogezea huduma hiyo karibu.

Thomas Munis, alisema hutumia gharama hadi shilingi 240,000 kwa ajili ya kupata leseni ya vilipuzi, na kwamba hutumia muda hadi wa wiki mbili kupata kibali.

“Tunatumia gharama kubwa hadi kwenda ofisi za madini makao makuu Dodoma kupata kibali cha vilipuzi kwa ajili ya shughuli zetu za madini… licha ya kutumia fedha nyingi, pia tunatumia zaidi ya wiki moja, huku shughuli za uchimbaji zikisimama tunaomba msaada serikali itusaidia kusogeza huduma karibu,” alisema Munis.

Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka, alisema mara kadhaa amekuwa akizungumza na wachimbaji hao na kwamba kilio chao ni kusogeza huduma ya utoaji leseni ya vilipuzi wilayani humo.

Alisema amelifikisha suala hilo kwa Waziri wa Madini, Dotto Biteko, na kwamba kinachosubiriwa ni utekelezaji.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon, alieleza hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na kuandika mapendekezo kwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ili kusogeza huduma hiyo karibu na wachimbaji.