Wachimbaji walia Tume ya Madini

11Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wachimbaji walia Tume ya Madini

MWENYEKITI wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula, amekutana na kilio cha wachimbaji wa madini mkoani Lindi, kuhusu ongezeko la tozo zilizo kinyume cha sheria ya madini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachimbaji hao walisema halmashauri za wilaya na vijiji zimekuwa zinawatoza tozo zaidi na ile iliyowekwa na sheria mama ambayo ni 0.03 badala yake wamekuwa wakitumia sheria ndogo zilizopitishwa na Baraza la Madiwani kuwatoza tozo zaidi kinyume cha sheria mama.

Waliongeza kuwa halmashauri zinatoza tozo zao, na halmashauri za vijiji nazo zinajipangia ushuru wao, hivyo kuwa kero na kusababisha usumbufu.

Kilio hicho walikiwasilisha wakati wa mkutano mkuu wa sekta ya madini uliofanyika tarehe Januari 22, 2019 chini ya uenyekiti wa Rais John Magufuli.

Prof. Kikula alikutana na kilio hicho akiwa ziara mkoani humo kutembelea na kukagua shughuli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wadau wa madini.

Kufuatia kilio hicho, Prof. Kikula alitoa wito kwa wachimbaji wa madini ya gypsum, kokoto, chumvi na mchanga nchini kote kuwa na subira wakati Tume ya Madini ikihangaikia utatuzi wa changamoto hiyo ya utozwaji wa tozo zinazo tozwa na baadhi ya halmashauri za wilaya na vijiji kinyume cha taratibu za sheria ya madini.

Prof. Kikula alitoa kauli hiyo baada ya kutembelea machimbo mbalimbali ya madini ya gypsum ikiwamo ya kampuni ya KNAUF Gypsum Tanzania Ltd, machimbo ya mavuji yanayomilikiwa na mchimbaji mdogo Faridu Sheweji na mchimbo ya chumvi yanayomilikiwa na Magereza Lindi eneo la Machole.

Akijibu hoja ya kero hiyo, Prof. Kikula alikiri uwapo wa malalamiko hayo kutoka kwa wachimbaji wa mikoa mbalimbali nchini na kuwa siyo kwa Lindi peke yake.

Alishangazwa na hali hiyo kwa kuwa sheria ya madini na miongozo mbalimbali iko wazi na inaelekeza vizuri kuhusu tozo zinazotakiwa kutozwa.

Alisema wanafanya jitihada kutatua kero hiyo, hivyo watawasilisha malalamiko yao kwa mamlaka ya juu ambayo ni Waziri wa Madini, Doto Biteko ili azungumze na Waziri wa Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo, ili kuondoa kero hiyo.

“Nalitambua hili tatizo, kila tunapofanya ziara mikoa mbalimbali hii changamoto inajitokeza, sijui ni kwa nini inakuwa hivyo kwa sababu sheria iko wazi namna tozo zinavyotakiwa kutozwa.

Naomba niwaahidi tutalishughulikia hili haraka sana, na mara baada ya ziara hii tutaandaa ripoti na kuiwasilisha kwa Waziri Biteko, pamoja na ripoti, lakini pia nitamwambia kwa mdomo ili kusisitiza juu ya kero hii,” alisema Prof. Kikula.

Prof. Kikula aliziomba halmashauri na kila mdau wa madini kote nchini wazisome na kuzipitia vizuri sheria ya madini hususani inayohusu tozo mbalimbali za madini kabla ya kuanza kuwatoza wachimbaji.

Aliambatana na Kamishna wa Madini, Prof. Abdulkarim Mruma, katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Njombe na Iringa kukagua shughuli za madini na kusikiliza na kutatua kero.

Habari Kubwa