Wadau kilimo waiafiki mbolea ya Microp

24Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau kilimo waiafiki mbolea ya Microp

MBOLEA mpya aina ya Microp ambayo ni mahususi kwa ajili ya kuongeza mavuno zaidi kwenye mazao ya mahindi na mpunga imepokewa kwa furaha na wadau wa kilimo katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kikao cha kujadili namna ya kumsaidia mkulima wa zao la mahindi pamoja na mpunga ili ajikwamue na kilimo cha ukosefu wa mavuno zaidi shambani, walisema mbolea ya Microp  inayotengenezwa na Kampuni ya Yara imekuja kuleta mageuzi makubwa kwa mkulima shambani na kuwa itamsaidia kuvuna mavuno zaidi pamoja na mazao kuwa na virutubisho aina tano tofauti ambavyo ni muhimu kwa ongezeko la tija kwenye kilimo cha zao la mahindi.

“Wakulima wetu wengi kwenye kilimo cha mahindi changamoto kubwa ni kwenye matumizi ya mbolea, ambapo wamekuwa wakitumia tu mazoea ambayo hupelekea mavuno kuwa hafifu shambani, lakini ujio wa mbolea ya Microp wakulima wataondokana na kupata mavuno machache ya gunia saba kwa hekali na kuongezeka hadi kufikia gunia 30 shambani,” alisema Dk. Juliana Mwakisindo, mtafiti na Meneja wa Tari Kifurilo wilayani Mufindi.

Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Damas Lubuva, alisema kampuni ya Yara Tanzania imeonyesha mafanikio makubwa ya kuwajali wakulima kwenye wilaya hiyo baada ya kuzindua ujio wa mbolea ya Microp na kwamba kama halmashauri watashirikiana na Yara kutoa elimu ya shamba darasa kwa wakulima ili waweze kuongeza tija katika kilimo cha mkono.

“Sisi kama halmashauri tunadhani hii mbolea itakuwa na manufaa makubwa kwa wakulima wetu, tunachoahidi ni kutoa elimu kwa wakulima, maofisa ugani pamoja na vyama vya ushirika waweze kuipokea vizuri, lakini ili tupate tija na kuongeza uzalishaji wa mazao mengi shambani kwa kweli tunashauri kitu cha kuanza nacho kwa sasa ni kwenye upimaji wa afya ya udongo, inatakiwa tujue afya ya udongo wetu na ikiwezekana hata mashamba darasa ambayo tutafanyia kazi afya ya udongo ingejulikana,” alisema Lubuva.  

Kwa mujibu wa Meneja Biashara wa kampuni ya Yara Tanzania Nyanda za Juu Kusini, John Meshack, mbolea ya Microp imelenga kumnyanyua mkulima mdogo wa chini kuvuna mazao mengi shambani na wanawashauri wakulima ambao wanamitaji midogo kuanza kutumia mbolea hiyo.

“Mkulima  mwenye mtaji mdogo tunamshauri aanze na mbolea hii ya Microp na baadaye aende kwenye mbolea ya Yaramila otesha kwa sababu zile mbolea nyingine hatuzitoi sokoni, na hii bidhaa mpya ya mbolea tunalenga asilimia 80 ya wakulima wa mahindi na mpunga ambao uwezo wao ni mdogo tunawaletea bidhaa ambayo siyo gharama kubwa kwa ili wapate matokeo chanya kwenye kilimo hivi sasa,” alisema Meshack.

Alieleza kuwa tangu mbolea ya Microp iingie sokoni katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini hadi sasa jumla ya tani 600 zimeshanunuliwa na wakulima katika muda wa wiki mbili wakiwamo wakulima wa Mkoa wa Songwe pamoja na wakulima wa Halmashauri ya Mji Mafinga mkoani Iringa.

“Mbolea hii inachakatwa hapahapa nchini na kiwanda kipo jijini Dar es Salaam hiyo yote ni kuwahudumia wakulima kwa karibu zaidi,” alisema.

Meshack alisema mbolea hiyo inavirutubisho vya Zinc na Sulphur Micronutrients ambazo  zinahitajika kwenye  mazao ili yaweze kuwa na  viwango vyenye bora.

Habari Kubwa