Wadau sekta kilimo waja mambo 10

01Jul 2019
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau sekta kilimo waja mambo 10

WAKATI serikali ikifanya maboresho ya sera ya kilimo ya mwaka 2013, wadau wa kilimo nchini wametoa mapendekezo katika maeneo 10 yanayopaswa kufanyiwa maboresho, mojawapo ni upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ansaf, Audax Lukonge.

Wakizungumza na waandishi wa habari Mjini Morogoro mwishoni mwa wiki, wadau hao wakiongozwa na Jukwaa huru la Wadau wa Kilimo (Ansaf), walieleza kuwa sera ya kilimo ya mwaka 2013 imekuwa na changamoto nyingi kwa wakulima nchini.

Baadhi ya wadau hao ni Chama cha Wakulima Tandahimba (Tafa), Action Aid Tanzania, Chama cha wafanyabiashara, wasindikaji na wasafirishaji wa mboga, viungo, matunda na maua nchini (TAHA), Mtandao wa asasi zisizo za kiserikali mkoani Arusha (Anglonet), Chama cha Maendeleo Mwanasatu (Mwado), Taasisi ya wajasiriamali vijijini, chama cha wafugaji jamii ya Kimaasai (MPDO-Lareto), pamoja na Katani Ltd.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ansaf, Audax Lukonge, alisema kwenye sera mpya inapaswa kueleza namna ya kudhibiti upotevu wa mazao wakati wa kuvuna.

“Tunashauri sera ihimize serikali na wadau waweke mkazo katika kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kupunguza upotevu wa mazao kwenye  mnyororo wa thamani, vipaumbele viwekwe katika kuhimiza upatikanaji wa elimu kwa wadau, teknolojia za uhifadhi, miundombinu ya uhifadhi katika maghala na vihenge,” alisema Lukonge.

Alisema sera mpya pia itambue umuhimu wa upatikanaji wa takwimu sahihi za kilimo na uwapo wa wadau mbalimbali, alisema kunapaswa kuboreshwa dawati la sekta binafsi pamoja na kuundwa  kwa dawati maalumu la vyama vya wakulima na ushirika kwa maendeleo ya kilimo.

Pendekezo lingine ni kuwapo kwa msukumo zaidi kwenye upatikanaji na matumizi bora ya mbegu na pembejeo muhimu za kilimo, huduma za ugani, tafiti, na matumizi bora na endelevu ya udongo kwa mazao mbalimbali ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Lingine ni serikali kutunga sheria ya kulinda ardhi ya kilimo, kutambua na kuheshimu maeneo yaliyotengwa mahsusi kwa shughuli za kilimo nchini, ambapo sheria hiyo iendane na mipango ya matumizi bora ya ardhi, hati miliki, mazao ya kipaumbele na mabadiliko ya tabia nchi.

Pia sera iweke mazingira rafiki yatakayohakikisha uwapo na ukuaji wa viwanda vya ndani kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo ya Kilimo (ASDPII) na mwongozo wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Kadhalika, sera iongeza nguvu kwenye mpango wa utekelezaji wa mkakati wa kushirikisha vijana kwenye kilimo biashara.

“Sera ya kilimo inatambua umuhimu wa miundombinu katika maendelo ya kilimo. Ili kukuza kilimo kunahitajika kuwekeza kwenye miundombinu ya nishati, umwagiliaji, usafirishaji wa mazao vijijini, masoko na hifadhi ya mazao na mashirika,” alisema Lukonge.

Alisema sera ya kilimo inatambua umuhimu wa kuongeza bajeti ya kilimo na bima ya mazao, hivyo serikali inapaswa kutoa asilimia 10 ya bajeti itakayokwenda kwenye kilimo pamoja na uharakishwaji wa kuanzisha bima ya mazao.