Wadau wa kilimo wampa 5 JPM TADB mikoani

17Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wadau wa kilimo wampa 5 JPM TADB mikoani

WADAU wa kilimo wamepongeza pendekezo la Rais John Magufuli la kutaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuwa na matawi mikoani ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na huduma nyingine za benki hiyo.

 

Rais alitoa pendekezo hilo alipokutana na wafanyabiashara kutoka nchi nzima Ikulu, jijini Dar es Salaam.

 

Wadau wamesifu pendekezo la rais kwa kusema benki hiyo ikiwa karibu na wateja wake na kutoa mikopo kwa wakati, jambo hilo litachochea kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi hapa nchini. Wamesema TADB ipo katika nafasi nzuri ya kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta ya kilimo jambo ambalo linahimizwa sana na Rais.

 

Akihojiwa juu ya maoni ya wadau wa benki yake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, amesema benki inayafanyia kazi kimkakati maelekezo ya Rais na kufafanua kwamba tayari ofisi zimefunguliwa katika baadhi ya mikoa.

 

Ameeleza kwamba tayari ofisi zimefunguliwa katika mji wa Kigoma na majiji ya Mwanza na Dodoma.

 

Ofisi ya Mwanza, ameeleza, ilifunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Machi 19, mwaka huu na inahudumia mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera.

Maandalizi ya mwisho yanafanywa kufungua ofisi katika Jiji la Mbeya, ameeleza kiongozi huyo, na kufafanua kwamba ofisi hiyo itahudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, na Ruvuma.

 

Ofisi ya Dodoma, amaeleza, imefunguliwa toka mwaka jana na ofisi ya Kigoma imekuwa ikuhudumia wakulima kwa miezi tisa iliyopita.

 

 

“Tunafarijika wadau wanapoeleza uhitaji wa huduma zetu na kutambua kazi yetu. Agizo la Rais linaimarisha dhamira yetu ya kuwa karibu na wananchi na linatupa hamasa ya kufungua ofisi mpya za kongani ili kuhudumia wateja wetu,” alisema Justine.

 

“Kama ulimsikiliza vizuri, Rais Magufuli ameonyesha kuguswa na utendaji kazi wa Benki ya Kilimo na ndiyo sababu anapenda ifungue matawi mikoani ili kusaidia serikali kuharakisha azima yake ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo 2025. Ujenzi wa viwanda msingi wake mkuu ni kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema Anangisye Mwakalindile, mkulima wa parachichi wa Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.

 

 Mwakalindile alikumbusha pia kwamba wakati akiwa katika ziara mkoani Mbeya, Rais Magufuli aliwaasa wakulima kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Benki ya Kilimo ili kukuza mitaji na kuinua kilimo nchini.

 

Samson Maduhu, mkulima wa pamba, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, alisema TADB ikiwa na matawi mikoani wakulima watanufaika na mikopo kwa kuongeza tija katika kilimo.

 

“Mimi nipo kwenye nafasi nzuri ya kuelezea umuhimu na faida ya kuwapo kwa benki hii kwani katika kipindi kifupi wakulima wengi wa pamba tumenufaika na huduma za benki hiyo kwa kupata pembejeo mbalimbali kwa urahisi na kwa wakati,” alisema Maduhu.

 

Evodius Barongo, mfanyabiashara wa kahawa wa Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera amliema wakazi wengi wa Kagera wameona umuhimu wa Benki ya Kilimo kupitia vyama vya ushirika. Benki imetoa mikopo ya zaidi ya bilioni 32 kwa ajili ya kukuza zao la kahawa.

Serikali inataka Tanzania ijenge uchumi wa kati wezeshi na unaotegemea viwanda ifikapo 2025.

 

Katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja TADB imerejesha matumaini kwa wadau wa kilimo nchini kwa kuwapatia mikopo ambayo imesaidia kuinua hali ya wakulima na kukuza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hapa nchini.

Habari Kubwa