Wadau wa zao la ndizi watakiwa kutumia njia sahihi katika uzalishaji

26Sep 2021
Mary Mosha
Moshi
Nipashe Jumapili
Wadau wa zao la ndizi watakiwa kutumia njia sahihi katika uzalishaji

WAZIRI wa Kilimo prosefa Adolf Mkenda, amewataka wadau wa zao la ndizi nchini wakiwemo wawekezaji kuzalisha zao hilo kwa tija kwa kutumia njia za kisasa ili waweze kukidhi viwango vya soko hilo nje ya nchi.

WAZIRI wa Kilimo prosefa Adolf Mkenda.

Akizungumza Jana wakati wa kufungua mkutano wa wadau wa ndizi wa Kanda ya Kaskazini uliofanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro amesema kwa sasa tayari serikali imepata masoko na kuwataka wakulima kulima kwa tija.

Amesema serikali kupitia Wizara ya kilimo ipo tayari kushirikiana bega kwa bega na wadau wote watakaojitokeza katika kuwekeza kwenye zao la ndizi.

"Tunapozungumzia zao la ndizi nchini Tanzania, limezoeleka kwa kula na kunywa tu, ila duniani ni tunda. Kuna tofauti kubwa sana kwa sisi tunavyolichukulia zao hilo na wenzetu, hivyo zao la ndizi linauwezo mkubwa sana wa kuwa zao la biashara, mashamba tunayo, tulime kwa tija, wataalamu wetu wapo watatuelekeza na tutapata faida kupitia zao hili," amesema Prof. Mkenda.

Nae Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe, amesema ufufuaji za zao hili utawasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi na kuongeza pato la halmashauri zetu.

"Wataalamu wa Kilimo wote wapo chini yangu, ni wajibu wenu wa kuhakikisha wakulima wanafuata sheria na kanuni za kilimo bora ili tuweze kukidhi hitaji la soko na kuongeza mnyororo wa thamani," amesema Prof. Shemdoe.

Pamoja na hilo, Prof. Shemdoe ameziagiza Halmashauri zote nchini kunakolimwa ndizi kujenga vituo vya kukusanya zao hilo kwa kuwawezesha vijana kinamama na watu wenye ulemavu kujishughulisha kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani.

Awali Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali ya mboga, maua na matunda-TAHA, Dk Jackline Mkindi, amesema lengo la mkutano huo ni kuonyesha hali halisi ya uhitaji wa ndizi ndani na nje ya nchi.

"Leo tumekutana hapa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, lengo ni kuona namna ya kufufua zao la ndizi na kuongeza mnyororo wa thamani, ikiwa ni sehemu moja wapo ya kumkomboa mkulima kwenye tatizo la mporomoko wa bei,"

Amesema ukilinganisha Tanzania na nchi nyingine za Afrika bado uzalishaji ni mdogo licha ya kuwepo kwa maeneo makubwa yenye rutuba kwa ajili ya Kilimo.

"Hatujaja Leo kuangalia matatizo yanayowakumba wakulima wa ndizi na badala yake tumekuja hapa kuangalia namna ya kukidhi uhitaji wa soko tulilolipata," amesema Dk Jackline.

Nao baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro akiwemo Profesa Patrick Ndakidemi, amesema wakulima katika maeneo yao wapo tayari kulima kwa tija ikiwa serikali itaweka mazingira bora ya upatikanaji wa mbegu bora za ndizi.

"Hii ni fursa ya pekee kwa wakulima wetu ambao walitegemea sana zao la kahawa ambalo linakabiliwa na matatizo mengi, Wizara msitusahau katika kuhakikisha mnafufua mifereji ya asili ili wakulima waweze kulima kwa tija na kwa kibiashara zaidi," amesema Profesa Ndakidemi.

Nao baadhi ya wakulima wa kibosho akiwemo Sabastian Mallya amesema ni vyema wakulima wakapewa elimu ya namna bora ya kulima kwa kupewa sheria za kulima na kupewa mbegu bora.

"Ardhi zetu zinakubali kulima zao hilo, hatuna mbegu mwafaka jambo ambalo tunaweza kushindwa kuingia kwenye soko la nje, ikiwezekana kujengwe kiwanda cha kuongeza thamani bidhaa za ndizi kabla ya kuzisafirisha, hii itasaidia mkulima kutopata hasara," amesema Mallya.

Habari Kubwa