Waelekezwa fursa za kujiajiri

16Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Waelekezwa fursa za kujiajiri

VIJANA  wametakiwa  kuchangamkia  fursa zilizopo ili kujikwamua  kiuchumi  badala ya kukaa kusubiri  ajira kutoka  taasisi za serikali na mashirika binafsi.

Mkuu  wa  Mkoa  wa  Tabora,  Agrey Mwanri, picha mtandao

Akizungumza  katika  warsha ya 24 ya watafiti  wa masuala ya uchumi iliyowakutanisha watunga sera  na  viongozi  wa serikali  za mitaa iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti  wa Kuondoa  Umaskini (Repoa), Mkuu  wa  Mkoa  wa  Tabora,  Agrey Mwanri, aliwataka vijana kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ili kujikwamua kiuchumi.

“Tutatoa mikopo kwa ajili ya vijana, ila tunataka tusikie wanafanya nini? Opportunity are never given, they are taken (fursa hazitolewi bali zinachukuliwa),” Mwanri alisema.

“Mtu  mvua ikinyesha anashangilia mvua mvua mvua, lakini unamuuliza  una tikiti ‘hapana’, una muhogo ‘hapana’, sasa unashangilia nini?” Mwanri alihoji.

Alisema kazi ya serikali ni kujenga mazingira mazuri ili vijana  wayatumie katika kujikwamua kiuchumi, na kwamba jukumu kubwa zaidi ni la wananchi wenyewe kuangalia mazingira yao na kuchangamkia fursa zilizopo na kutokutarajia watu wengine kufikiri zaidi kwa niaba yao.

Alieleza kuwa Serikali Mkoa wa Tabora inafanya jitihada za kuhakikisha fedha iliyoelekezwa katika kutengwa  kwa ajili ya makundi maalum inatengwa kama ilivyoelekezwa  ili kuwakwamua wananchi  kiuchumi.

“Sasa hivi tunakwenda kwenye azimio la Kaliua, tumezungumzia  sasa  utaratibu  ambao  unahakikisha kundi hili la vijana  linapata  hiyo asilimia nne na kundi la kinamama linapata asilimia nne na kundi la walemavu linapata asilimia nne,”  Mwanri alisema.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Prof.  Faustin Kamuzora, alishauri kuangaliwa  upya  kwa mfumo wa elimu  nchini  tofauti na uliopo sasa ambao unawafanya vijana  kujianda kisaikolijia kuajiriwa  kuliko kutumia maarifa aliyonayo kujiajiri.

“Tuangalie upya mfumo wetu wa elimu kwa kuwa  fikra wanazojengewa  vijana  sio  sahihi,” Prof. Kamuzora  alisema.

Naye  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi, Dk. Avemaria Semakafu, alisema  maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mabadiliko mengi katika mfumo wa ufanyaji kazi, hivyo alitaka kufikiriwa upya kuhusu suala la  ajira nchini kwa kuwa mazingira ya sasa ni tofauti na zamani.

“Tunahitaji  kufikiria upya kuhusu  hili neno  ajira kutokana na ukuaji wa teknolojia hivi sasa, zamani mtu aliweza kualika vibarua wengi kulima shamba, kwa sasa trekta moja inaweza kufanya kazi  ya watu wengi,”   Dk. Semakafu alisema.

Habari Kubwa