Wafanyabiashara Ilala wachekelea Ilamaco kwa kunyang'anywa zabuni

04Mar 2016
Yasmine Protace
Dar
Nipashe
Wafanyabiashara Ilala wachekelea Ilamaco kwa kunyang'anywa zabuni

WAFANYABIASHARA katika soko la Ilala jijini Dar es Salaam, wameupongeza uongozi wa halmashauri hiyo kwa kuwanyang'anya zabuni ya kukusanya mapato Muungano wa Vyama vya Ushirika Soko la Ilala (Ilamaco).

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.

Ilamico inadaiwa imekuwa ikikusanya ushuru wa soko hilo, lakini inashindwa kuliboresha.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema licha ya kutoa ushuru wa Sh. 1,000 kila siku, hali ya soko ni mbaya na kipindi mvua wateja hushindwa kufika hapo kununua bidhaa.

Walisema Ilamico wapo katika soko hilo kwa miaka sita, lakini wameshindwa kuliboresha na kuwafanya wafanyabiashara kufanya kazi katika mazingira magumu.

“Tumekuwa tukilalamikia sana suala hilo, hatimaye Mungu ametupa majibu na hivi sasa amepatikana mkandarasi ambaye awali alikuwa akichukua ushuru na alifanikiwa kuliweka soko katika hali nzuri,” alisema mmoja wafanyabiashara hao ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake litajwe nakuongeza:

“Lakini fitna zilifanywa na viongozi wa soko na kusababisha mkandarasi huyo kunyang’anywa zabuni.”

Katibu wa Soko la Ilala, Ally Mbinga, alithibitisha Ilamaco kunyang’anywa zabuni katika soko hilo.

“Mwanzoni mkandarasi General Works alikuwa akichukua ushuru na hali ya soko ilikuwa nzuri na usafi ulikuwa ukifanyika, lakini kutokana na chuki, mkandarasi huyo alinyang’anywa zabuni na kuchukuliwa kwa Ilamaco,” alidai mfanyabiashara huyo.

Ofisa Hhabari wa Manispaa hiyo, Tabu Shahibu, alisema kuwa mkandarasi aliyepewa zabuni katika soko hilo, ana vigezo vyote na alikuwa akipeleka Sh. milioni 37 kwa mwezi.

Hata hivyo, alisema Ilamaco iliyositishiwa zabuni kwa sasa, walikuwa wakipeleka Sh. milioni 27 ila hao waliositishiwa walikuwa wakipeleka Sh. milioni 27 kwa mwezi.

“Si kweli kuwa alikuwa akileta Sh. milioni 16, mchakato wa zabuni umefanyika na huyo ndiye amepata zabuni hiyo,” alifafanua Ofisa huyo Habari wa Manispaa ya Ilala.

Habari Kubwa