Wafanyabiashara mabati wakaidi agizo la TBS

19Mar 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Wafanyabiashara mabati wakaidi agizo la TBS

SIKU chache baada ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kukamata zaidi ya mabati 2,000 ya migongo mipana yaliyotengenezwa chini ya kiwango jijini Mbeya na kuzuia yasiuzwe tena, wazalishaji na wafanyabiashara wamekaidi agizo hilo kwa kuendelea kuyasambaza kwa kuwauzia wananchi wa vijijini.

Baadhi ya vijana wakipakia mabati yasiyokuwa na viwango kwenye moja ya gari jijini Mbeya kwa ajili ya kwenda kuyaharibu baada ya maofisa wa Shirika la Viwango nchini (TBS), kubaini mabati hayo kuendelea kuuzwa. PICHA: NEBART MSOKWA

Hayo yalibainika juzi wakati wakaguzi ubora wa TBS kutoka makao makuu na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walipofanya ukaguzi kwenye viwanda vya kuzalisha bidhaa hiyo na kwenye maghala ya kuhifadhia ambapo walibaini mabati hayo yakiendelea kuuzwa.

Kufuatia hali hiyo shirika hilo liliamua kubeba mabati hayo na kwenda kuyahifadhi kwenye ghala maalumu kwa ajili ya kusubiria taratibu zikamilike ili kuyaharibu.

Wataalamu hao walibeba bati 2004 walizozikamata awali walipofanya ukaguzi kwenye viwanda viwili vya Dragon Mabati, Alaf limited na kwenye ghala la Kampuni yenye asili ya China ya Yalin International ambalo lilikutwa na mabati mengine zaidi ya 1,000 ambayo yalikuwa yameletwa baada ya msako wa awali.

Mkaguzi ubora mwandamizi wa TBS kutoka makao makuu, Mhandisi Donald Manyama, alisema walibaini kuwa bati hizo zenye migongo mipana za kiwango cha gage 30 zinaendelea kuuzwa maeneo ya vijijini walipofanya ukaguzi wa kushtukiza wilayani Rukwa.

Alisema baada ya kubaini hali hiyo waliamua kurudi Mbeya kwa ajili ya kuzihamisha kutoka kwenye maeneo ya viwanda na maghala walikozuia zisiuzwe na ndipo wakaamua kuzibeba na kwenda kuzihifadhi wenyewe.

Alisema shirika hilo lilibaini kuwa bati hizo zinaendelea kuzalishwa na kuuza baada ya kukagua katika ghala la Yalin na kukuta shehena mpya ya mabati zaidi ya 1,000 yakiwa yameingizwa kutoka jijini Dar es Salaam.

Ofisa Uhusiano wa TBS kutoka Makao Makuu, Roida Andusamile, aliwataka wananchi kuacha kununua bati hizo kwa madai kuwa zitawasababishia hasara kubwa kutokana na kuharibika baada ya muda mfupi.

Alisema aina hiyo ya bati kwa mujibu wa sheria haziruhusiwi kuzalishwa wala kuuzwa kwa wananchi na hivyo akawataka wazalishaji kuacha kukiuka masharti ya leseni zao akidai kuwa vitendo hivyo vitawaingiza hasara kubwa.

Alisema mabati ya aina hiyo yanaruhusiwa kuendelea kuzalishwa kwa kiwango cha kuanzia gage 28 kushuka isipokuwa kwa bati za kawaida ambazo wazalishaji wanaruhusiwa kutengeneza hata gage 32.

“Sisi hatuishii tu kuzichukua na kwenda kuziharibu bali tunatoa na elimu maana baadhi wanauza bila kujua kuwa bidhaa hizo hazina viwango vinavyotakiwa, kwa sasa tunaondoa bidhaa zote hafifu hata kama sio kosa la muuzaji,” alisema Roida.

Aliwataka wauzaji wa jumla kuwasiliana na wazalishaji wa bidhaa wanazoziuza pale wanapobaini kuwa ni hafifu ili wawarejeshee fedha zao au wawabadilishie na kuwapatia bidhaa zenye viwango vinavyostahili.

Naye Mkaguzi Ubora kutoka TBS, Baraka Mbajije, alisema wataendelea na zoezi hilo la ukaguzi katika mikoa ya Iringa na Njombe na kwamba lengo lao ni kuhakikisha wananchi wanatumia bidhaa zenye ubora unaostahili kwa viwango vya nchi.

Hata hivyo wakati wataalamu hao wakiendelea na zoezi hilo, yaliibuka mabishano kati yao na watumishi wa Kampuni ya Yalin International ambao walikuwa hawataki mabati hayo yachukuliwe na waligoma kufungua ghala mpaka wataalamu wa TBS walipotishia kuwafutia leseni.

Habari Kubwa