Wafanyabiashara madini wahakikishiwa usalama

23May 2019
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Wafanyabiashara madini wahakikishiwa usalama

MKUU wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Elizabeth Kitundu,
amewahakikishia wafanyabiashara wa madini usalama na kuwapo kwa
usiri wa kutosha katika biashara hiyo, ili wapate fedha na kulipa
kodi halali kwa serikali.

Kitundu alisema hayo jana mjini hapa wakati akizindua soko la madini
la Wilaya ya Babati lililoanzishwa rasmi na kuwekwa katika jengo la
Halmashauri ya Mji wa Babati, kwa ajili ya kuwahudumia
wafanyabiashara hao.

 

“Niwahakikishie kutakuwa na usiri wa kutosha na usalama utakuwa
wa uhakika kwa wauzaji wa madini watakaofika soko hili. Cha msingi
tunaomba ushirikiano wa watu wote na muwe wazalendo na wachapakazi
ili mkipata kipato chenu na serikali hakikisheni inapata sehemu yake
kwa ajili ya maendeleo ya taifa,” alisema.

Alisema anaamini kuwa baada ya kuzinduliwa kwa soko hilo, wachimbaji
wengi watajitokeza kwenda kutafuta leseni ili waanze kuchimba
kihalali na masoko hayo yatapunguza utoroshaji wa madini na
kuongeza ajira.

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa kuanzishwa kwa soko la madini kutakuwa  mkombozi kwa halmashauri kwa sababu zitapata ushuru hasa zile ambazo madini
yanapatikana, hivyo zitaondokana na kulalamika kuwa madini
yanazalishwa kwao na zenyewe haziambulii kitu.

Naye Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Manyara, Mhandisi Joseph
Kumburu, alisema soko hilo litakuwa linatoa huduma
siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kwa wiki. Alisema leseni
79 ndizo zinamilikiwa na Halmashauri ya Babati.

Ofisa Madini Mkaazi Mkoa wa Kimadini Mirerani, Daud Ntalima,
aliwaambia wadau wa madini kuwa serikali ilianzisha soko
la madini ili wachimbaji walipe kodi, kuwa na taarifa za
uzalishaji na kupata masoko ya madini.

“Serikali inawathamini sana wachimbaji wa madini, hivyo na nyie
muithamini serikali kwa kulipa kodi ili kuletewa huduma za
kijamii zilizo bora katika maeneo yenu na kuanzishwa kwa masoko,
kutawasaidia kupata fursa nyingi za kiuchumi,’’ alisema Ntalima.

Mwenyekiti wa wachimbaji Mkoa wa Manyara, Jastin Nyari, alisema kwa
sasa wana masoko ya ndani na alitumia fursa hiyo kuiomba serikali
iwapatie masoko ya nje pia huku akisisitiza kuwa hakuna mtu
atakayetorosha madini wakati kuna soko hilo.

Mwenyekiti wa Masoko ya Kimataifa kutoka Chama cha Wafanyabiashara wa Madini  (Tamida), Abe Latif Suleman,
alisema kuanzishwa kwa masoko ya madini, kutaepusha mlolongo wa
kodi, huku akisema madini ni ya pili kwa kuingiza kipato baada ya 
sekta ya utalii.