Wafanyabiashara wa China waonyeshwa fursa

14May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wafanyabiashara wa China waonyeshwa fursa

WAFANYABIASHARA wa China wametakiwa kuwekeza katika usindikaji wa mazao ya chakula kwa kutumia malighafi inayopatikana nchini ili kutosheleza mahitaji ya soko ifikapo mwaka 2050 ambapo inakadiriwa asilimia 50 ya watu barani Afrika watakuwa wamekimbilia maeneo ya mijini.

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki.

Wito huo ulitolewa na Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki, wakati akifungua kongamano la uwekezaji kati ya China na Tanzania katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), jana.

 

Kairuki alisema kuwa mahitaji ya chakula yatakuwa makubwa kutokana na ongezeko kubwa la watu wanaokimbia uchumi wa vijijini wa kilimo na kwenda mijini kutafuta kazi za viwandani na huduma.

 

Alisema Tanzania ina ardhi nzuri yenye rutuba pamoja na maji ya kutosha, hivyo kuwezesha uzalishaji wa mazao yanayotumiwa sana na jamii barani Afrika kama vile nafaka, maharage, mihogo, viazi vitamu na matunda ya aina mbalimbali yakiwamo maparachichi.

 

”Tanzania ina kila kitu na hamtahitaji kuleta mazao kutoka nje kwani kwa ardhi iliyopo na maji kuna uwezekano mkubwa wa kulisha kwa chakula majirani zetu kutokana na mahitaji yaliyopo,” alifafanua.

 

Aidha, Kairuki alisema  fursa nyingine ni usindikaji wa nyama pamoja na samaki ambapo alibainisha kuwa kuna mahitaji makubwa sana kwa soko la nchi za Asia.

 

“Lazima uwekezaji wenu ujikite katika viwanda, lakini kubwa kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini,” alisema.

 

Kairuki alisema mpaka sasa Tanzania ina soko la uhakika kutokana na kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye watu milioni 152 na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yenye watu milioni 800.

 

Akizungumzia biashara kati ya China na Tanzania, Kairuki alisema imekua kutoka dola za Marekani bilioni 3.9 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 7 kwa mwaka jana.

 

Alifafanua kwamba kuongezeka kwa kasi kwa biashara na uwekezaji kutachangia katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

 

Alisema uchumi wa Tanzania hivi sasa unakua kwa kasi ikiwa ya nchi ya tano katika bara la Afrika.

 

“Hali ya mazingira ya uwekezaji ni nzuri na ina fursa katika sekta za madini, kilimo, viwanda, ufugaji na sekta ya utalii kutokana na kuwapo kwa rasilimali za kutosha katika maeneo yote ya nchi,” alisema.

 

Aidha, aliwataka wafanyabiashara wa China kuingia ubia na wenzao wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya gesi asilia, makaa ya mawe, uchimbaji wa madini, utalii, sekta ya hoteli na nyumba za malazi katika hifadhi za taifa.

 

Alisema ni matumaini ya Tanzania ni kuona makampuni kutoka China yanakuja kwa wingi kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwamo ya miundombinu

 

Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka China unaongozwa na Mwenyekiti wa Makampuni ya Touchroad International Holding Group kutoka Jimbo la Zhejiang, Liehui.

 

Kongamao hilo limeshirikisha wafanyabiashara zaidi ya 60 kutoka China na 90 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Habari Kubwa