Wafanyabiashara, wachuuzi waiomba serikali kuwasaidia wasivunjiwe

16Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Morogoro
Nipashe
Wafanyabiashara, wachuuzi waiomba serikali kuwasaidia wasivunjiwe

WAFANYABIASHARA wadogo na wachuuzi zaidi ya 500 katika soko la Nanenane mjini hapa, wameiomba serikali kuingilia kati mgogoro ulioibuka baina yao na Manispaa ya Morogoro ambao wametangaza kuvivunja vibanda vyao na kuondoka katika eneo hilo.

Wamesema kitendo cha manispaa hiyo kutaka kuvunja vibanda vyao na kuwaondoa katika eneo hilo bila kuwaeleza sehemu ya kuwapeleka, kinaweza kuzuia vurugu na hivyo kuiomba serikali kuingilia kati ili kupata muafaka.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Ally Mndeme, alisema wanashangazwa na hatua ya manispaa kutaka kubomoa vizimba vyao wakati walikabidhiwa na uongozi wa kata kwa makubaliano ya ujenzi wake ili kufanya biashara katika eneo hilo.

“Mpaka tunajenga hivi vizimba tulikubaliwa na uongozi wa kata hii kwa kuwa eneo hilo walilitenga kwaajili ya kufanya biashara, lakini sasa tunashangazwa na manispaa kututaka kubomoa na kuondoka katika eneo hili, ina maana hawana mawasiliano na ofisi yao ya kata mpaka tumemaliza kujenga,” alisema.

Mfanyabiashara Lita Mathias, alisema hawapo tayari kuondoka katika eneo hilo kwa kuwa wameshaingia gharama za ujenzi wa vizimba hivyo ambavyo uongozi wa kata lilipo soko hilo, ulishabariki.

Alisema wanakusudia kuifikisha manispaa hiyo mahakamani endapo watabomoa vizimba vyao kwa kuwa waliruhusiwa kihalali na uongozi wa kata na mpaka kufikia hatua ya kujenga na kufanya biashara katika eneo hilo.

Akizungumzia malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, John Mgalula, alisema manispaa imepanga kuwaondoa wananchi wote wanaofanya biashara katika maeneo ambayo hayaruhusiwi ikiwemo soko hilo ambalo eneo hilo halikutengwa kwa ajili ya kufanyia biashara.

Habari Kubwa