Wafanyabiashara walipa faini mil. 60/- kukwepa kifungo

07Dec 2018
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Wafanyabiashara walipa faini mil. 60/- kukwepa kifungo

MFANYABIASHARA maarufu mkoani hapa Kamaljit Hanspaul (58) na wenzake watatu wamenusurika kwenda jela miaka mitatu baada ya kulipa faini ya Sh. milioni 60 kukwepa kwenda jela.

Hanspaul alilipa faini ya Sh. milioni 30 na wenzake watatu Kumar Vemula (27), Vinoth Krishanth (29), raia nchini India na Raiph Leopold Hruscka (54), raia wa Ujerumani, walililipa faini ya Sh. milioni 10 kila mmoja.

Akisoma hukumu hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Arusha jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Niku Mwakatobe, alisema washtakiwa hao walikutwa Novemba 12, mwaka huu, kwenye kampuni ya Hanspaul Automech wakifanya kazi bila vibali vya kazi.

Alisema kutokana na makosa hayo mahakama imemhukumu (Hanspaul) kulipa faini ya Sh. milioni 30 kwa makosa matatu ya kuajiri wafanyakazi watatu wa kigeni bila kuwa na vibali vya kazi au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela kama atashindwa kulipa faini hiyo.

Pia washtakiwa wengine watatu ambao ni raia wa kigeni wamehukumiwa kulipa faini ya Sh. milioni 10 kila mmoja kwa kosa la kufanya kazi nchini bila kuwa na vibali vya kazi au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela.

Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Khalili Nuda, aliwasomea maelezo ya awali na washtakiwa walikiri kufanya makosa hayo.

Kwa upande wa Wakili wa Utetezi, Salimu Mushi, aliiomba mahakama hiyo kupunguza adhabu kwa sababu washtakiwa hao ni mara ya kwanza kukutwa na hatia na raia hao wa kigeni walikuwa wakifuatilia vibali.

Mapema washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 4, mwaka huu na kusomewa mashtaka yao ambapo Vemula na Hruscka walikuwa wanafanya kazi kwenye kampuni ya Hans Paul Automech kama wahandisi washauri wa kiwanda hicho, ambapo Krishanth anafanya kama mhandisi wa magari.

Watuhumiwa hao walitiwa mbaroni Novemba 12 mwaka huu na Kamishna wa Kazi nchini, Gabriel Malata, alipofanya ziara katika kiwanda hicho.

Habari Kubwa