Wafanyabiashara wataka mipaka isifungwe

07Feb 2016
Gurian Adolf
Nipashe Jumapili
Wafanyabiashara wataka mipaka isifungwe

WAFANYABIASHARA mkoani Rukwa wameiomba serikali kuacha kufunga mipaka kwa lengo la kuzuia biashara ya mazao kwenda nchi jirani kwani kufanya hivyo kunawasababishia hasara kubwa.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao katika ukumbi wa mikutano wa Liboli Center mjini Sumbawanga, mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara, wakulima na wamiliki wa viwanda (TCCIA) mkoani humo, Sadriki Malila alisema kila mwaka serikali imekuwa ikifunga mipaka kwa lengo la kuwazuia wakulima na wafanyabiashara kutafuta soko la mahindi nchi jirani kwa hofu ya kupata baa la njaa. Alisema kitendo hicho kinasababisha wakose soko la mazao hayo wakati serikali haina uwezo wa kununua mahindi yote yaliyozalishwa katika msimu. Matokeo yake, alisema Malila, wakulima hubaki nayo na kuishia kuharibika kwa kuwa hawana namna bora ya kuhifadhi na hivyo kusababisha hasara. Malila alisema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imekuwa ikitegemea mazao ya chakula kutoka hapa nchini, lakini serikali imefunga mipaka na hivyo biashara na nchi hiyo ya jirani kushindwa kufanyika. Mwenyekiti huyo wa TCCIA alisema kama serikali itaendelea kuzuia kuuza mazao katika nchi jirani, ijitahidi kuyanunua mazao hayo yote kwa bei ya soko la wakati huo. Aidha alitaka serikali iache kuwakopa wakulima ili kuwasaidia kupata fedha kwa ajili ya kuendelea na kilimo cha mazao ya chakula. Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Said Magalula ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo alisema pamoja na kukosekana soko la uhakika la mahindi hayo, wakulima wasife moyo. Aliwataka wajitume zaidi katika kuzalisha chakula kwani serikali inaendelea na jitihada za kutafuta masoko. Alisema kuwa ni kweli kuwa kama wakulima na wafanyabiashara watapewa fursa ya kuuza mazao katika nchi jirani itawasaidia kupata fedha, lakini hawana budi kuzalisha ziada ili serikali iweze kulitazama kwa jicho la pekee ombi lao hilo. Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanalipa kodi ili serikali iweze kupata fedha za maendeleo, ikiwemo za kununua mahindi hayo.

Habari Kubwa