Wafanyabiashara watakiwa kujiunga huduma bima afya

26Mar 2020
Boniface Gideon
Kilindi
Nipashe
Wafanyabiashara watakiwa kujiunga huduma bima afya

WAFANYABIASHARA wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, wametakiwa kujiunga na bima za afya ili kuwa na uhakika wa matibabu.

MENEJA wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Tanga (NHIF) Ally
Mwakababu kushoto akitoa elimu kwa mfanyabiashara wa viatu wilayani
Kilindi kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya wakati wa uhamasishaji wananchi juu ya vifurushi vipya katika halmashauri ya wilaya hiyo.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tanga, Ally Mwakababu, wakati akitoa elimu juu ya faida ya kujiunga na bima za afya kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama ‘machinga’.

Mwakababu alisema mwanzo wananchi walikuwa na dhana kuwa mifuko ya bima za afya ilikuwa ni kwa wafanyakazi walioajiliwa.

“Tumekuja kuwaambia kuwa bima ya afya ni kwa watu wote na sio waajiliwa pekee…tunawapa elimu wafanyabiashara kuwa ili uweze kuendeleza biashara yako na usifirisike, ni lazima uwe na uhakika wa matibabu," alisema Mwakababu.

Alisema familia nyingi zimeingia kwenye matatizo kutokana na gharama kubwa za matibabu.

“Sasa hivi tuna fao la jipimie, ndio maana tumekuja kuzungumza na nyie wananchi kuwa matibabu ni gharama kubwa, hivyo ni vyema mkajiunga na bima ya afya, " alisema Mwakababu.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilindi, Bakari Mkalakala, aliwaomba wadau na watumishi wa umma kuhakikisha wanashirikiana na wananchi katika utoaji wa elimu juu faida ya kujiunga na bima za afya.

Alisema CCM katika wilaya wamejipanga kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya faida ya kujiunga na NHIF.

"Niwaombe viongozi wa CCM wilaya yetu kuanzia ngazi za chini muwaelimishe wananchi juu ya faida ya kujiunga na bima za afya na mimi nitazunguka kutoa elimu hii," aliongeza Mkarakala.

Baadhi ya wafanyabiashara waliishukuru serikali kwa kuwafikia wananchi wa maeneo ya vijijini kupata elimu juu ya faida za bima ya afya.

"Tunashukuru sana kwa hili la kuletewa elimu hii, sisi tulioko huku vijijini hatujawahi kufikiria kwamba tutakuja kufikiwa na huduma hizi… ila tunaomba gharama za bima zipunguzwe kidogo ili sisi wanyonge tumudu," alisema Salehe Mhina.

Habari Kubwa