Wafanyakazi wa hoteli waomba kurudishwa kazini

30Jun 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Wafanyakazi wa hoteli waomba kurudishwa kazini

BAADHI ya wafanyakazi wa hotelini visiwani hapa wamedai kuwa licha ya serikali kuruhusu shughuli zote kurejea baada ya kupungua kwa janga la corona bado hawajaruhusiwa kurudi kazini.

Wakizungumza na Nipashe, walisema kuwa tangu kuingia kwa janga la corona wamepewa likizo bila ya malipo na hakuna kiwango chochote cha fedha wanachopatiwa.

Wahid Khamis, ambaye ni miongoni mwa wafanyakazi hao aliiomba Wizara ya Kazi kuhakikisha wanarejeshwa kazini ili waendelee kufanya kazi na kupata kipato.

“Kwa kweli corona tunaambiwa imeisha, lakini bado hali za kiuchumi ni ngumu maana kazini tumepewa likizo bila  malipo wala hatujui likizo hiyo itaisha lini,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana (Zanzibar Youth Forum), Maulid Suleiman, aliitaka Serikali ya Zanzibar kuwasaidia vijana waliowekeza katika sekta ya utalii ambao kwa sasa hawana ajira kufuatia kujitokeza kwa athari za ugonjwa wa corona na hoteli kushindwa kupokea wageni kwa zaidi ya miezi minne sasa.

Alisema sekta ya utalii imeathirika vibaya na ugonjwa wa corona na vijana waliowekeza katika sekta hiyo ikiwamo wafanyakazi wa hoteli, wasambazaji wa vyakula hotelini na watembezaji wa wageni wamepoteza ajira kwa zaidi ya miezi minne sasa.

Alisema licha ya serikali kuruhusu kuanza kwa sekta ya utalii kwa kuingia kwa wageni nchini, bado hali haijawa nzuri kutokana na nchi zingine za Ulaya ugonjwa wa corona upo.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Mkunazini Zanzibar, Dk. Michael Hafidh, alisema tayari wameanza maandalizi ya kupokea wageni na watalii wanaozuru kanisa hilo baada ya shughuli hizo kufungwa kwa zaidi ya miezi minne kutokana na janga hilo.

Alisema zaidi ya vijana 20 wamekosa kazi katika kipindi cha miezi minne ya kufungwa kwa shughuli za kutembeza watalii katika eneo la kanisa la Mkunazini Unguja na kuathirika kiuchumi.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk. Mohamed Abdalla, alisema tayari serikali imeruhusu kuanza kwa shughuli za utalii kwa ndege kubwa kuja moja kwa moja kutoka Ulaya.

“Matarajio yetu makubwa kuona shughuli za huduma za utalii zinarudi kama kawaida kwa ndege kubwa kuanza safari zake...najuwa itachukua muda kidogo kwa sababu wenzetu Ulaya ugonjwa bado upo,” alisema

Habari Kubwa