Wafugaji nyuki wapewa mbinu kuepuka umaskini

22Sep 2020
Grace Mwakalinga
Songwe
Nipashe
Wafugaji nyuki wapewa mbinu kuepuka umaskini

VIKUNDI vitano vya wafugaji wa nyuki katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe vimepatiwa mafunzo ya namna bora ya ufugaji, mizinga na soko ili waweze kujikwamua na umaskini.

Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Shanta Gold Mine (New Luika) ndio iliyovisaidia vikundi hivyo kuwapatia mizinga, mafunzo na soko baada ya kuona hawanufaiki na ufugaji wa nyuki.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa vikundi hivyo, Kaimu Meneja wa Shanta Gold Mine (New Luika), Exupery Lyimo, alisema kampuni hiyo iliviwezesha vikundi hivyo, ili sasa waanze kupata faida na kuweza kujikwamua na umaskini kutoka maeneo ya Saza na Mbangala.

Alisema kampuni hiyo ilianza kuviwezesha vikundi hivyo mwaka 2017 kwa kuanza kuvipa mizinga ya nyuki na kwamba kampuni yenyewe ndio mnunuaji wa asali ambazo zinazalishwa na vikundi hivyo.

Lyimo alisema baada ya kuanzisha vikundi hivyo kampuni ya Shanta ilitoa jumla ya mizinga 250 kwa vikundi hivyo katika maeneo ya Saza na Mbangala pamoja na mashine 10 zinazotumika kuvuna asali.

"Mkuu wa Wilaya ya Songwe, alitufuata sisi wadau wa maendeleo ili tuone ni kwa namna gani tunashirikiana na jamii katika eneo la ufugaji nyuki, pamoja na kutoa mizinga hiyo, pia tuliwaleta wataalamu wa nyuki kutoka Tabora kwa ajili ya kutoa elimu," alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah, alizitaka taasisi za kifedha wilayani humo kupunguza masharti ya kukopa ili vikundi hivyo vinufaike na mikopo bila kuumia.

"Ufugaji wa nyuki ni fursa, hivyo nawasihi wafugaji mzingatie elimu mliyopewa ili mfuge kisasa na kupata faida kwa sababu mmehakikishiwa soko na kampuni hii,”  alisema Jeremiah.

Habari Kubwa