Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, nyama waomba kupewa ranchi

08Feb 2016
Nipashe
Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, nyama waomba kupewa ranchi

WAFUGAJI wa ng’ombe wa maziwa na nyama Kanda ya Mashariki, wameishauri Serikali kuwatengea ranchi ndogondogo ili waweze kufuga kisasa na kiushindani.

Mbali ya ranchi, wafugaji hao wameiomba serikali iwatafutie masoko ya uhakika, kuwajengea majosho na kudhibiti dawa feki na chanjo za magonjwa ya mifugo.

Wafugaji hao walisema hayo wakati wakipokutana Mjini Morogoro kupitia yaliyomo kwenye mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya mifugo.

Baadhi ya wafugaji Shambakubwa Longido na Optat Lyimo, walishauri maeneo ya wafugaji kutengwa kwa kugawanywa kama ranchi ndogo ndogo na kwamba jambo hilo linawezekana kwa kugawanya mashamba pori ambayo hayajaendelezwa.

“Nilifanikiwa kugawiwa eneo la ekari 250 katika ranchi ya Dakawa, nafuga kisasa ng’ombe wa maziwa na nyama, kwa utaratibu huu unasaidia kuongeza ushindani na maendeleo ya wafugaji na sekta ya mifugo…tunahitaji pia mbegu za kisasa za mifugo,” alisema Shambakubwa.

Wafugaji hao pia waliiomba serikali kusimamia upatikanaji wa chanjo ya magonjwa ya kuambukiza magonjwa ya miguu na midomo, homa ya mapafu na upele.

“Soko limevamiwa na dawa feki (bandia), tunaamini Serikali ikituuzia madawa yenyewe na kutuwekea majosho, dawa na chanjo tutakazotumia zitakuwa ni za uhakika na salama,” alisema Lyimo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Anusiata Njombe, alisema Serikali imeweka mpango mkakati wa kuinua na kuendeleza sekta ya mifugo katika maeneo 15 ya kimkakati ili iweze kutoa mchango stahiki kwenye pato la taifa.

Habari Kubwa