Wafugaji wanufaika kiwanda cha maziwa

01Aug 2020
Renatha Msungu
Arusha
Nipashe
Wafugaji wanufaika kiwanda cha maziwa

WAFUGAJI mkoani Arusha, wamenufaika na kujengwa kwa kiwanda cha maziwa cha Kilimanjaro Fresh baada ya kuwa na uhakika wa kuwa na eneo la kupeleka bidhaa zao za maziwa, ambazo awali zilikuwa zinaharibika.

Wamesema mikataba walioingia na kiwanda hicho imewasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza kipato chao.

Teddy Sulle, mmoja wa wafugaji mkoani hapa, alisema Kilimanjaro Fresh imewasaidia kwa kiasi kikubwa kuinuka kiuchumi kwa kuwa sasa maziwa yao hayaharibiki tena kwa kukosa soko.

Alisema wanakishukuru kiwanda hiko na serikali kwa kuwa karibu na wenye viwanda ambao nao wanakuwa karibu na wafugaji.

Mkurugenzi wa Kilimanjaro Fresh, Irfhan Virjee, alisema kiwanda hiko kina mpango wa kuanza kupeleka maziwa Kenya ili kupanua soko la bidhaa zake.

Alisema lengo lao ni kuanza kuzalisha lita 30,000 kwa siku tofauti na sasa wanazalisha lita 10,000 kwa siku kutokana na ufinyu wa soko, akiongeza kuwa mkakati huo unalenga kuinua kipato cha wafugaji wa Mkoa wa Arusha na mikoa jirani.

"Tanzania ni wa pili kwa ufugaji wa ng'ombe barani Afrika. Kwa hiyo, tunapaswa kuwa juu hata katika uzalishaji wa maziwa," alisema Virjee.

Daktari wa Mifugo, Banson Ng'aida, alisema siri kubwa ya ng'ombe kutoa maziwa ni lishe bora na usafi kwa mifugo inayofugwa katika mazizi na wafugaji wengi wanakwama kupata maziwa mengi kutokana na kufeli katika eneo hilo.

Habari Kubwa