Wafugaji wapewa kibano

09Jan 2017
Gurian Adolf
SUMBAWANGA
Nipashe
Wafugaji wapewa kibano

SERIKALI mkoani Rukwa imepiga marufuku watendaji wote wa vijiji kuruhusu mifugo kutoka ndani ya mkoa huo.

Badala yake mwenye mifugo aonyeshe kibali cha kupokelewa kule anakoelekea kikionyesha kukubaliwa kutoka kwa uongozi wa sehemu anayokwenda.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven, alisema bila mfugaji kuonyesha kibali cha kupokelewa anakokwenda hatakubaliwa kwa sababu wengi wamekuwa na vibali vya anakotoka tu, hivyo ni lazima awe na kibali cha anakokwenda ili kuepusha kupeleka matatizo sehemu nyingine.

Vilevile, alisema viongozi wa vijiji wa mkoa wa Rukwa wasiwe wanapokea mifugo inayoingizwa katika mkoa huo bila kumpa mfugaji kibali kinachompokea kikionyesha anakwenda kijiji gani na kama kuna eneo la yeye kufugia na kulisha mifugo hiyo.

Steven alisema kuwa agizo hilo amewapa wakuu wa wilaya zote nne za mkoa huo ili kudhibiti uingiaji wa mifugo katika mkoa huo ambao una matukio ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji na tayari kuna watu wamepoteza maisha.

Alisema kwa watakaopuuza agizo hilo na kupokea mifugo kinyemela, serikali haitasita kuwachukulia hatua kwani wao ndiyo chanzo cha migogoro baina ya wafugaji na wakulima inayotokea mkoani humo.

Aliongeza kuwa wafanyabiashara wa minadani nao waache mtindo wa kuingia na mifugo mingi kwa madai kuwa wanapeleka minadani, lakini hawauzi mifugo hiyo kisha kuibakiza mkoani humo, hivyo kuanzisha migogoro na wakulima.

Kadhalika, alisema hivi sasa mkoa wa Rukwa umeamua kujipanga vizuri ili kumaliza kabisa migogoro baina ya makundi hayo mawili na miongoni mwa njia watakazotumia ni kuhakikisha sheria inafuatwa kwani kuna baadhi ya watendaji wanapindisha sheria na kuwa tatizo katika kumaliza migogoro hiyo.

Habari Kubwa