Wafugaji watakiwa ushirikiano kufanikisha mkakati ufugaji kisasa

24Nov 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wafugaji watakiwa ushirikiano kufanikisha mkakati ufugaji kisasa

WAFUGAJI wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili kufanikisha mkakati wa miradi ya ufugaji wa kisasa wa ng'ombe bora wa maziwa na nyama laini na ngozi nzuri kwa ajili ya soko la uhakika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabliel, ndiye aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, wakati akizindua kampeni ya uhimilishaji wa ng'ombe katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Uhimilishaji huo ulifanyika Kata ya Bugwema na kuhudhuriwa na viongozi wa wilaya hiyo, wafugaji, wawakilishi kutoka ofisi ya mbunge wa Musoma Vijijini na wadau wengine wa sekta ya mifugo.

Prof. Ole Gabriel alisema, lengo la uhimilishaji huo ni upandikizaji kwa kuweka mimba kwenye ng'ombe wa kienyeji kwa kuweka mbegu za ng'ombe wa kisasa kwa njia ya mrija ili kuongeza ubora na wingi wa mifugo.

"Wafugaji toeni ushirikiano kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuanzisha miradi ya ufugaji wa kisasa wa ng'ombe bora wa maziwa na nyama laini na ngozi nzuri kwa ajili ya soko la uhakika," Prof. Ole Gabriel alisema.

Alisema ni muhimu wafugaji kuzingatia maelekezo yanayotolewa na serikali ili kuachana na ufugaji wa mazoea, badala yake watoe ushirikiano ili kufanikisha mpango huo wa uhimilishaji.

"Kuwa na ng'ombe ni utajiri, hivyo wafugaji wanatakiwa kuwa tayari kuzingatia maelekezo ya serikali, kwa kuwa ina lengo la kuwasaidia kunufaika na utajiri wa mifugo walionayo," alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk.  Vincent Anney, alisema, ofisi yake kwa kushirikiana na idara ya mifugo, watafanyia kazi kilichosemwa na katibu huyo, kwa kuhimiza wafugaji kufuata maelekezo ya serikali.

"Kwa niaba ya wakazi Wilaya ya Musoma wakiwamo wafugaji, tunakushuru na tunaahidi kufuata maelekezo ulioyatoa kwa wafugaji kwa kuwahimiza waendelee kuyazingatia ili wanufaike," alisema Dk. Anney.

Alisema, Kata ya Bugwema ni miongoni mwa kata 21 za wilaya hiyo yenye wafugaji wengi wa ng'ombe na kwamba ndiyo maana uhimilishaji umefanyika eneo hilo.

Habari Kubwa