Wafundishwa kukabiliana na viwavijeshi

11Jun 2019
Godfrey Mushi
 MOSHI
Nipashe
Wafundishwa kukabiliana na viwavijeshi

WATAALAMU wa sekta ya kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, wameanza kuwajengea uwezo wananchi wa vijiji sita vya Kahe Mashariki kuhusu namna ya kukabiliana na viwavijeshi aina ya ‘fall armyworm’ wakati huu wa msimu wa masika.

Viwavijeshi hivyo wenye jina la kisayansi 'spodoptera frugipedra' ndio wadudu hatari zaidi wanaoharibu mazao ya chakula.

Akithibitisha wataalamu hao kufika katika vijiji hivyo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima kuhusu udhibiti wa viwavijeshi hao iwapo watajitokeza kushambulia mazao, Diwani wa Kahe Mashariki (CCM), Kamili Mmbando, alisema wataalamu hao wameshawafikia robo tatu ya wakulima.

Hayo yamo katika taarifa maalum ya maendeleo ya kata hiyo yaliyosomwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wanaounda halmashauri hiyo.

Kwa mujibu wa Ofisa Kilimo wa Halmashauri hiyo, Chikira Mcharo, viwavijeshi hivyo hupenda kula mahindi machanga na wana uwezo wa kula baadhi ya mimea mingine.

Mazao mengine yanayoshambuliwa na viwavijeshi hao ni mchele, mtama, ngano, miwa na mboga.

Asili ya wadudu hao ni nchi zilizo katika maeneo ya kitropiki kwenye Bara la Amerika Kaskazini na Kusini.

Taarifa zaidi za kisayansi zinaeleza kuwa viwavijeshi aina ya ‘fall armyworm’, huzaana na kuongezeka wakati wowote wakiwa katika hatua zozote za maisha.

‘Fall armyworm’ ni viwavi na ila si minyoo kama vile jina lao linavyojieleza na hatua yao ya maisha ya mdudu kamili huwa ni nondo au kipopo.

Habari Kubwa