Wafurahia kuuza mazao kiushirika

17Jun 2021
Nebart Msokwa
Kyela
Nipashe
Wafurahia kuuza mazao kiushirika

​​​​​​​WAKULIMA wa kakao katika Wilaya ya Kyela, wamekiri kuwa utaratibu wa kuuza zao hilo kupitia vyama vya ushirika una tija kuliko utaratibu waliokuwa wanautumia awali ambao ulikuwa unawaumiza.

Wakizungumza na Nipashe juzi, baadhi ya wakulima hao walisema mfumo wa kuuza mazao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi gharani umewasaidia kupanda kwa bei ya zao hilo kutoka kati ya Sh. 2,000 na 2,500 za awali mpaka Sh. 4,500 na hadi 5,000.

Mmoja wa wakulima hao, Simon Andongolile, kutoka Kanjunjumele alisema mfumo wa awali ulikuwa unaruhusu madalali ambao walikuwa wanawaumiza wakulima na kwamba walikuwa hawana nafasi ya kuonana na wanunuzi moja kwa moja.

Alisema kwa sasa mkulima anauza kakao zake kulingana na bei iliyoko sokoni na akibaini kuwa bei hiyo haina faida kwake anaamua kuacha mpaka itakapotoka bei nzuri.

“Lakini mfumo huu pia unaisaidia serikali kukusanya mapato yake vizuri. Kwa  mfano sasa hivi kwa taarifa za mrajis ni kwamba halmashauri yetu imekusanya zaidi ya Sh. milioni 1.3 ambazo awali zilikuwa zinapotea,” alisema Andongolile.

Naye Erick Kabombo alisema mfumo wa uuzaji wa zao hilo kupitia vyama vya ushirika imesaidia kuzalisha ajira kwa vijana ambao wanafanya kazi ya kubeba maginia na kuyapanga kwenye maghala.

Alisema awali walikuwa wanauza kakao ikiwa mbichi, hivyo kutengeneza mazingira ya kuwaibia mazao yao kwenye kutokana na vipimo vilivyokuwa vinatumika.

“Pia tunanufaika kupitia vyama vyetu vya ushirika ambapo tunapata bima za afya ambazo zinatusaidia kwenye matibabu mwaka mzima, tunaiomba serikali iendelee kusimamia mfumo huu,” alisema Kabombo.

Mrajisi wa Msaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mkoa wa Mbeya, Angela Maganga, alisema zao hilo linalimwa katika halmashauri tatu za mkoa huo ambazo ni Kyela, Rungwe na Busokelo na kwamba mfumo wa ushirika una faida nzuri.

Alisema kwa sasa kakao hizo zinauzwa kwa njia ya mnada ambapo kampuni zinashindanishwa ili kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri.

Habari Kubwa