Wahasibu waonywa kuabudu umangimeza

13Jan 2019
Robert Temaliwa
Bagamoyo
Nipashe Jumapili
Wahasibu waonywa kuabudu umangimeza

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, amewataka wahasibu wa Halmashauri za Chalinze na Bagamoyo, kuacha kukaa ofisini badala yake wafike kwenye vyanzo vya mapato ili kujionea hali halisi ya sehemu husika.

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, picha mtandao

Mkuu wa wilaya alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya ushauri ya wilaya (DCC).

Kawawa alisema kazi ya kukusanya fedha inahitaji ufuatiliaji hivyo ni wajibu wa wakuu wa idara kuhakikisha wanafuatilia walipa ushuru kwenye vyanzo ili kujiridhisha endapo malipo wanayolipa yanalingana na kile walichobeba au kuzalisha.

Alisema suala la kuongeza mapato ndani halmashauri zote mbili linatakiwa kupewa kipaumbele kwani fedha zinazopatikana za ushuru zinaweza kusaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizopo ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa.

Awali Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao, akisoma taarifa ya utendaji kazi za halmashauri hiyo, alisema mapato yameendelea kukua mwezi hadi mwezi na kufikia Shilingi milioni 600 kwa mwezi wa Oktoba na Novemba 2018 kutoka Shilingi milioni 400 kwa mwezi Julai 2018.

Milao alisema ongezeko hilo limetokana na juhudi za mkuu huyo wa wilaya kutokana na kufuatilia kwa karibu vyanzo vya mapato na namna watumishi wa halmashauri hiyo wanavyokusanya hali iliyoleta msukumo na kuongezeka kwa mapato.

Aliongeza kwa kutaja changamoto zinazowakabili katika kufikia lengo wanalokuwa wamelikusudia kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wafanya biashara juu ya ulipaji kodi ya huduma za mji pamoja na uhaba wa vyombo vya usafiri.

Alisema halmashauri imejiwekea mikakati ya kuhakikisha inaendelea kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kulipa kodi ya huduma na kuwachukulia hatua wale wote wenye madeni sugu.

Pamoja na taarifa hiyo mkuu wa wilaya alionyesha kutoridhishwa na mapato hayo na kutaka kasi iongezwe katika ukusanyaji ili kufikia Shilingi milioni 900 kutoka milioni 600 za sasa.

Kawawa alisema tayari ameshafanya uchunguzi na kubaini fedha nyingi zinapotelea kwenye mifuko ya watu na kwamba hatokubali mapato ya halmashauri yafanyiwe ufisadi.

Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote mbili za Chalinze na Bagamoyo kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato na kwamba ikitokea mkuu wa idara husika anazembea katika kufuatilia na kukusanya mapato atahakikisha anamuwajibisha.

Habari Kubwa