Wahimizwa kulipa kodi bila shuruti

05Jan 2017
Dege Masoli
Tanga
Nipashe
Wahimizwa kulipa kodi bila shuruti

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka wananchi kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi bila shuruti na kufanya hivyo si tu kutimiza
wajibu, bali pia ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za jamii nchini.

Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Swalehe Byarugaba, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Nipashe kuhusiana na changamoto mbalimbali
zinazoikabili mamlaka hiyo katika kukusanya kodi za serikali.

Byarugaba alitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa
ujumla wa kuwataka walipe kodi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wameungana na Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya umaskini.
Aliwataka wananchi kutambua kuwa mambo makubwa yaliyoahidiwa na
serikali katika kuondoa kero na kujenga misingi imara ya uchumi
yanategemea pamoja na mambo mengine ukusanyaji wa kodi kazi
inayofanywa na TRA.Aidha, alisema wadau wasiione mamlaka hiyo kama adui na badala
yake wajenge urafiki nayo ikiwa ni pamoja na kufuata sheria, kupata
ufafanuzi wa mambo yasiyoeleweka vema na hata kuwasiliana nayo katika
masuala mbalimbali yanayohusu kodi.Hata hivyo, Meneja huyo alielezea aina tatu za kodi zinazolalamikiwa zaidi na wadau kuwa ni za umiliki wa mali aliyonayo mteja, usajili ambayo hulipwa mara moja tu na ile ya mapato inayotokana na gari au
chombo husika kufanya kazi.


Byarugaba alifafanua kuwa ada ya umiliki ambayo kimsingi ndiyo kero
kubwa inayolalamikiwa na watu wengi inayotozwa kwa mwenye magari kila
mwaka na kwamba ada hiyo haiangalii kama chombo husika kinafanya kazi
au hakifanyi.

Alieleza kuwa wamiliki wengi wamekuwa hawaelewi msingi wa ada hiyo, jambo linalosababisha malalamiko mengi na kwamba yanatokana na
wahusika kutofuata taratibu, kanuni na sheria za ada hiyo.

Alisema sheria za ada hiyo inaelekeza kuwa endapo gari imekufa, mmiliki atoe taarifa polisi na vielelezo.
Alisema baada ya polisi kupitia vielelezo hivyo na kujiridhisha, mteja atalazimika kuiandikia barua mamlaka hiyo pamoja na viambatanisho hivyo ikionyesha kuwa gari hiyo haifanyi kazi na haimiliki tena na hivyo anaomba ifutwe.

“Mamlaka ikipata barua na viambatanisho hivyo na kujiridhisha kabla ya kufuta umiliki, huangalia kama mteja ana madeni ya nyuma au la….hapo tunafuta umiliki na hatuwezi kumfuata tena aliyefuata utaratibu huo. Lakini watu hawafuati na badala yake wanazusha malalamiko tu,” alisema Byarugaba.

Habari Kubwa