Wahitimu gesi, mafuta wapewa neno

07Dec 2017
Christina Mwakangale
Nipashe
Wahitimu gesi, mafuta wapewa neno

NAIBUMakamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Cuthbert Kimambo, amewataka wahitimu wa shahada ya pili ya masuala ya gesi na mafuta kuitumia taaluma yao vizuri ili Watanzania wanufaike na rasilimali hiyo.

NAIBUMakamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Cuthbert Kimambo

UDSM kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Norway (NTNU) kiliwapeleka wanafunzi tisa kupata mafunzo hayo kwa ufadhili wa kampuni ya utafutaji gesi na mafuta ya Statoil.

Prof. Kimambo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya mahafali ya nne ya kuwapongeza wahitimu hao baada ya kuhitimu shahada hiyo Norway. 

Alisema wakati sekta hiyo ikiibukia, kuna haja ya wataalamu kuwa wazalendo na ni Watanzania wachache waliofanikiwa kufikia hatua hiyo.

“Ushirikiano kati ya Tanzania na Norway umewaongezea ujuzi na nguvu wataalamu wetu katika sekta hii kupitia programu ya Anthei ambayo ni mahsusi kwa kufadhili wanafunzi kusoma kozi hii,” alisema Prof. Kimambo.

Meneja Mkuu wa Statoil nchini, Oysten Michelsen, alisema lengo la kushirikiana na vyuo vikuu ni kujengea uwezo wanafunzi ili kumudu shughuli za sekta hiyo.

“Kupitia mafunzo haya tunashirikiana na vyuo vikuu kujengea uwezo wanafunzi na ufundishaji kwa maendeleo endelevu ya sekta hii,” alisema Michelsen.

Mmoja wa wahitimu, Zuhura Mkindi, alisema wataitumia vyema taaluma hiyo ili kulinufaisha taifa.

 

 

Habari Kubwa