Wahoji manufaa gawio la mashirika

03Dec 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Wahoji manufaa gawio la mashirika

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamehoji Zanzibar kutofaidika na mgawo wa fedha za gawio la mashirika ya umma kwa taasisi zenye sura ya Muungano.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, picha mtandao

Hilo liliibuliwa jana na Mwakilishi wa Mpendae, Mohamed Said Dimwa, aliyetaka kujua mgawo wa mashirika ya umma unaofanyika Tanzania Bara unainufaishaje Zanzibar.

Mwakilishi huyo alihoji wakati wa kikao cha Baraza la Wawakilishi huku akitaka kujua gawio la mashirika hayo linainufaishaje Zanzibar.

Dimwa alisema hivi karibuni Rais John Magufuli alipokea gawio la fedha za mashirika ya umma zaidi ya Sh. bilioni 2.75 yakiwamo mashirika yenye sura ya Muungano na fedha zake hukusanywa zikitokea Zanzibar katika vyanzo vyake vya mapato.

“Kutokana na fedha hizo, Zanzibar inanufaikaje kwa sababu baadhi ya mashirika yanayotoa gawio yana sura ya Muungano?” Alihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, alisema ziko taasisi za Muungano zilizoko Zanzibar ambazo huchangia gawio la fedha zinazoingia katika mfuko mkuu wa serikali.

Aliyataja mashirika hayo kuwa ni Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Shirika la Posta (TPC).

“Tumefanya mawasiliano na wenzetu wa Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuulizia kuhusu suala la mgawo wa fedha zinazotokana na gawio kwa taasisi na mashirika ya umma ambayo ni ya Muungano,” alisema.

Habari Kubwa