Wajasiriamali wa nafaka, maziwa, rangi wanolewa

11Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Kahama
Nipashe
Wajasiriamali wa nafaka, maziwa, rangi wanolewa

WAJASIRIAMALI wa nafaka, maziwa, rangi, asali na unga lishe, wamepatiwa elimu kuhusiana na taratibu za kufuata ili kupata leseni ya kutumia alama ya ubora ya TBS kutokana na huduma hiyo kuwa inatolewa bure kwa wajasiriamali.

Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga, PICHA MTANDAO

Elimu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki kwa wajasiriamali wilayani Kahama, mkoani Shinyanga na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Akizungumza wakati wa utoaji elimu hiyo wilayani hapa, Ofisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, alisema katika semina hiyo wajasiriamali walionyeshwa kufurahishwa na elimu waliyoipata na waliahidi kutuma maombi TBS na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania

(TFDA), ili kuomba wataalamu wa nafaka kwenda kuwapa elimu juu ya madhara yatokanayo na upakaji mafuta kwenye michele na njia sahihi ya kuandaa nafaka zao.

Mtemvu, alisema wamelenga wajasiriamali kwa kuwa ndilo kundi muhimu katika kukuza uchumi, hivyo alitoa wito kwao kutumia fursa zinazotolewa na shirika hilo kukuza thamani ya bidhaa zao.

Aliwataka wajasiriamali kujitokeza kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kwa kuwa gharama zote zinabebwa na serikali.

Hivi karibuni Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga, alisema katika kipindi cha Septemba na Desemba, mwaka jana wajasiriamali 13 walithibitishiwa ubora wa bidhaa yao, hivyo kufanya idadi yao waliopata vyeti vya ubora na leseni ya kutumia alama ya ubora kufikia 440.

Alisema tayari wajasiriamali waliothibitisha ubora wa bidhaa zao zimeendelea kupenya kwenye masoko ya SADC na EAC. Alitoa mwito kwa wajasiriamali kuchangamkia fursa hiyo. Ili kufikia wengi zaidi, Msasalaga, alisema hivi karibuni wanatarajia kutoa elimu kwa wajasiriamali kwenye kanda nne ili kuwahamasisha kuchangamkia fursa hiyo.

Wakati huo huo, Mtemvu, alisema maofisa wa shirika hilo wameendelea na Kampeni yake katika Wilaya ya Kahama kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kununua bidhaa zilizothibitishwa na TBS na jinsi gani wajasiriamali wanaweza kupata leseni ya TBS bure bila gharama yoyote.

Kampeni hiyo ya elimu kwa umma imefanyika maeneo ya Soko Kuu, Stand Kuu na Shule ya Msingi Malunga Mjini Kahama. Wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo sambamba na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo ubora wa bidhaa.

Habari Kubwa