Wajasiriamali, wafanyabiashara watakiwa kuchangamkia fursa

17Jun 2019
Elizaberth Zaya
DAR
Nipashe
Wajasiriamali, wafanyabiashara watakiwa kuchangamkia fursa

MFUKO wa uwezeshaji wa wafanyabiashara Afrika (AECF) umewaomba wajasiriamali na wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji, ili kuongeza ajira kwa idadi ya watu na kusaidiana na serikali kukuza zaidi uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa wadau wa uwekezaji kutoka katika mabara ya Amerika, Ulaya na Afrika jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa AECF Tanzania, Gerald David, alisema sekta binafsi ndiyo inatoa ajira nyingi , hivyo lazima kuongeza nguvu katika sekta hiyo kuhakikisha  inatoa huduma kwa idadi kubwa ya watu mijini na vijijini na kuongeza zaidi ajira.

Alisema upo umuhimu kwa wawekezaji kupanua zaidi wigo wa uwekezaji hususan katika maeneo ya kilimo, nishati na maeneo mengine ambayo yanasaidia kutoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi kuanzia wa hali ya chini.

“Tunaona kwamba nchi za Afrika zimekuwa zikitumia bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi hizo, wakati kuna uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula cha kukidhi mahitaji yote, ilhali tuna vyanzo vingi ikiwamo nishati mbadala za kukidhi mahitaji na ambazo ni nzuri kwa kukidhi mazingira, tutumie fursa hizi hizi kunufaika wenyewe,” alisema David na kuongeza:

“Sisi kama AECF ambao ni wadau muhimu katika sekta ya uwekezaji hususani katika nchi za bara la Afrika, tumeamua kushirikiana na serikali ya Tanzania kwa kuiunga mkono hasa kipindi hiki inapoimarisha na kujenga uchumi wake kupitia viwanda. Tunataka wajasiriamali na wafanyabiashara watumie fursa hii kuwekeza katika kilimo pamoja na rasilimali zote zilizopo Tanzania,” alisema David.

Aliongeza: “Kama ni katika kilimo tuone.” Alisema AECF  imeanza kuwawezesha wakulima  na wanaowekeza katika nishati mbadala na kwa Tanzania pekee imetoa Dola za Marekeni milioni 60 sawa na Shilingi bilioni 1.38 kwa ajili ya kuwezesha kampuni 71, na zaidi ya watu milioni 1.7 wamenufaika na msaada huo.

Mjasiriamali, Fahad Awadh ambaye ni mfanyabiashara wa korosho kutoka Zanzibar, alisema tatizo kubwa linalochangia watu wengi kuagiza bidhaa kutoka nje ya Tanzania ni kutokana wafanyabiashara wengi wa ndani kushindwa kuongeza thamani katika bidhaa  zao ili kuziweka katika hali ya mvuto.                                         

Habari Kubwa