Wajasiriamali wahoji M50/- za Magufuli

27Feb 2016
Leonce Zimbandu
Dar
Nipashe
Wajasiriamali wahoji M50/- za Magufuli

WAKATI Rais John Magufuli akiendelea kujipanga kutekeleza ahadi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ya kutoa Sh. milioni 50 katika kila kata, kikundi cha wajasirimali cha mtaa wa Yangeyange kata ya Msongola wilaya ya Kinondoni, wameomba serikali iharakishe kutoa mitaji hiyo.

Rais John Magufuli.

Ombi hilo limetolewa na wakazi hao mwishoni mwa mafunzo ya siku tatu ya ujasirimali, ambapo walieleza ukosefu wa mitaji ya kuendeleza biashara zao.

Mmoja kati ya wanakikundi, Yasinta Kapangamwaka, alisema wameamua kujipanga kupata elimu hiyo mapema ili kuunga mkono ahadi ya Rais Maguguli ya kuwainua wafayabiashara ndogondogo ambao wamejiunga kwenye vikundi.

"Tunaomba serikali ya awamu ya tano kutekeleza ahadi zake kwa wajasirimali kwa kutoa mitaji," alisema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Epejesta iliyotoa mafunzo hayo, Julias Zumba, alisema alianzisha kampuni hiyo kwa lengo la kusaidia wajasirimali wanaoishi pembezoni mwa miji mikuu.

Alisema tangu wameanza kutoa mafunzo hayo mapema mwaka huu, wamefundisha wajasirimali 1,675.
"Tunatoa elimu hiyo bure, hivyo tunaomba serikali kuunga mkono juhudi hizi ili elimu waliyopata wanavikundi wasiijutie," alisema.

Katibu toka ofisi ya diwani wa kata ya Msongola, Mrisho Goha, alisema ofisi ya kata imejipanga kuanzisha vikundi hivyo ili kurahisisha utoaji wa mikopo.

"Tumeanza kuandaa vikundi kwa kushirikiana na Afisa Maendeleo wa kata, Theodora Kavishe ili kuangalia namna ya kuwasaidia kuondoa umaskini," alisema.

Habari Kubwa